VIJANA PANGANI WANUFAIKA NA MAFUNZO YA SDGs


Vijana takribani mia moja (100) kutokea wilayani Pangani mkoani Tanga wamepatiwa mafunzo kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu huku wakifanya idadi hiyo kufikia elfu Sitini (60,000) kwa waliopatiwa mafunzo kwa nchi nzima.

Hayo yamesemwa na Afisa Habari kutoka Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa Didi Nafisa, wakati akizungumza na kituo hiki katika mazungumzo maalum ndani ya Studio zetu.

Awali Afisa habari huyo kutoka kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa, ameanza kwa kumnukuu mwakilishi Mkazi Umoja wa Mataifa Alvaro Rodriguez kwamba namna gani vijana wa Pangani watasaidiwa licha ya utofauti wao wa kifikra, mitazamo na shughuli zao.


Amesema kuwa wanatembea Duniani kuwaambia vijana kuhusu SDGs yaani Malengo ya Maendeleo endelevu ya Dunia, pamoja na kuwaelezea ujumbe wa matumaini, iwapo malengo ya Dunia yatafanyiwa kazi.

“Alvaro anasema kwa miaka 15 ambayo imepita Umoja wa Mataifa umekuwa ukizungumzia Malengo ya Milenia na hivi sasa tunazungumzia Malengo ya Dunia, lakini utofauti uliopo tumeona kwamba wakati wa Malengo ya Milenia haikuwa ikifahamika vizuri malengo haya ni kitu gani hasa kwa jamii na ndio maana sasa tulivyofika katika Malengo haya ya Dunia tunatembea tukiwaambia vijana kuhusu malengo ya dunia na ujumbe wa matumaini ambao malengo hayo umeubeba, kwamba Dunia ni namna gani inaweza ikawa huko mbeleni iwapo malengo ya dunia yatafanyiwa kazi"

Ameongeza kuwa “Pia mfumo ambao tunautumia wakati wa kufundisha vijana, ni kwamba watakuwa wanatumia elimu waliyoipata kuwaelezea wengine kwa kujitolea, watakuwa wanajitolea kuwaelezea wengine kwamba malengo ya dunia ni kitu gani, tunatumaini kwamba iwapo wataweza kujitolea na kuwaelezea wengine ujumbe huu utasambaa na kuwafikia watu wengi zaidi”. Amesema Mwakilishi Mkazi Umoja wa Mataifa


Bi. Nafisa amesema kuwa licha ya kwamba hawajawahi kufika Tanga kwa ujumla, lakini vijana zaidi ya elfu sitini tayari wameshawafikia nchini, hivyo wamepania kuwafikia watu wote ili kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma.

“Tangu tulipoanza mwaka 2016 mpaka sasa hivi tumeshatoamafunzo kwa takribani zaidi ya vijana 60,000 Tanzania, kwasababu hatujawahi kufika Pangani na Tanga kutoa mafunzo hayo hii itakuwa ni mara ya kwanza lakini tumeshatembea zaidi ya mikoa kumi na tumekuwa tukitembea mashuleni, vyuoni tukiongea na vijana ambao tunasema wako nje ya mfumo wa elimu (Youth out school), tumeongea na asasi mbalimbali”.

Amesema “Kwahiyo tunajaribu kufikia kila mtu kwasababu kauli mbiu ya malengo ya dunia inasema (Leave No One Behind) ni kuhakikisha kwamba hakuna mtu ambaye anayeachwa nyuma. Kwasababu katika moja ya lengo ya malengo ya Dunia ni kuhakikisha kila mtu anafahamu, na inatarajia kwamba kila mtu ataweza kuyafikia. Kila mtu kila nchi itaweza kuyatimiza, na kuweza kuyatimiza ni lazima tuhakikishe kila mmoja anafahamu “hakuna anayeachwa nyuma”.


Kwa upande wake Bi Rebeca Gyumi ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Msichana Initiative, amezungumzia namna ambavyo mpaka sasa vijana na kila mtu anavyoshiriki kutekeleza malengo ya kidunia aidha kwa kujua ama hata bila kujua.

“Unajua malengo ya maendeleo endelevu ni namna tu ambavyo serikali,  kwasababu ukiangalia umoja wa mataifa ni serikali hizi zimeamua kuungano, ziliamua tu kuweka maneno ili kusema haya ndiyo malengo yetu 17 lakini kimsingi sisi hapa wote kwa namna moja au nyingine tulishakuwa tayari tunafanya vitu vinavyoendana na moja ya malengo yale”. 

Mafunzo kwa vijana wilayani Pangani umemkutanisha pia mwakilishi Mkazi Umoja wa Mataifa Alvaro Rodriguez ambaye huu ni ujuo wake wa pili,  ambapo pamoja na mambo mengine amezungumza na mabinti Wilayani humo ili kujua changamoto zao na namna ya kuwasaidia kufikia kwa pamoja Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Bwana Alvaro Pangani, ameambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Msichana Initiative Bi Rebeca Gyumi pamoja na baadhi ya wawakilishi kutoka Ubalozi wa China hapa Nchini.

Mwenyeji wa mafunzo hayo ni Mkuu wa wilaya ya Pangani Mheshimiwa Zainab Abdallah Issa pamoja na viongozi wengine wa kiserikali pamoja na halmashauri ya wilaya ya Pangani.

No comments

Powered by Blogger.