TATIZO LA MATUNDU YA VYOO SHULE YA MSINGI PANGANI LAWAKUTANISHA WADAU


Katika kukabiliana na tatizo la upungufu wa matundu ya vyoo kwenye shule ya msingi Pangani uongozi wa kata ya Pangani Magharibi umekutana na wadau wa maendeleo ili kujadili namna ya kutatua tatizo hilo.

Akisoma taarifa  Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Mwalimu Hamisi Mohamed amewaeleza wadau hao kuwa tatizo la upungufu wa matundu ya vyoo shuleni hapo lichukuliwe kuwa la dharura kwani choo kilichopo chenye matundu kumi na nne yaani wasichana matundu saba na wavulana matundu saba, kimekuwa kibovu na kina nyufa jambo ambalo linaweza kupelekea madhara.

“Ndugu wadau wa elimu, shule ya msingi Pangani choo kilichopo chenye matundu 14 chenyewe kimekuwa kibovu na kina nyufa kubwa kitu ambacho kinaweza kusababisha hatari hapo baadaye, lakini pia tumepata msaada wa choo chenye matundu sita kutoka Islamic Help lakini mpaka sasa hakijakamilika, ziko chemba ambazo hazijafungwa pia mtiririko wa maji bado haupo”. Amesema Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Pangani.

Pamoja na kuelezea makubaliano ya kikao hicho Mwenyekiti wa Maendeleo ya kata ambaye ni Diwani wa kata hiyo John Semkande, amesema wamewashirikisha wadau ili kuona namna ya kutatua changamoto hizo.

 “Kwahiyo tumeamua kuwaita wadau leo kuwashirikisha ili kuona ni namna gani kama jamii tunaweza tukatatua ile changamoto ya matundu 14 yale ili kuweza kuvijenga upya, tumekubaliana tumshirikishe afisa ujenzi ili afanye tathmini ili tujue gharama ni kiasi gani halafu tutawaambia wadau, lakini baadae tutawashirikisha wananchi kupitia vikao vyetu”. Amesema Diwani wa kata ya Pangani Magharibi John Semkhande.

Wilaya ya Pangani iliyopo Mkoani Tanga inakabiliwa na upungufu wa Matundu ya vyoo katika shule mbalimbali, huku Shule ya msingi Pangani pekee ikiwa na upungufu wa matundu ya vyoo 53.

No comments

Powered by Blogger.