YALIYOJIRI KWENYE KIKAO CHA BARAZA LA MADIWANI WILAYANI PANGANI



Uhamasishaji wananchi katika kuchangia ujenzi wa kitua cha afya cha Mwera wilayani Pangani umesitishwa hadi pale wataalam wanaosimamia ujenzi huo watakapokabidhi mpango kazi wa ujenzi wa kituo hicho.

Suala hilo limeibuka wakati wa kikao cha Madiwani wilayani Pangani kilichofanyika hivi karibuni ambapo limezua vuta ni kuvute kwa baadhi ya madiwani walipokuwa kwenye kikao hicho hali iliyosababisha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani Mheshimiwa SEIF ALLY kutumia sheria ya kupigia kura kwa ajili ya maamuzi  ya kuhamasisha au kutokuhamasisha wananchi kuchangia ujenzi huo ambapo baada ya kupiga kura waheshimiwa madiwani kwa pamoja wameamua kusubiri  mpango kazi huo yaani BOQ kutoka kwa wataalam.

“Wanao sema twendeni  kwa wananchi tukaanze kuwaelemisha leo, alafu BOQ itafuata baadae kama maelezo ya utetezi ya katibu wangu alivyosema kwamba tuacheni na shughuli zimeshaanza kufanyika, sawa?  wanyooshe mikono juu, haya kura tano hizo. Haya wanaosema mpaka tupate BOQ ndio twende kwa wananchi kura kumi hizo kwahiyo mchakato huu tunausimamisha mbaka tupate BOQ. Amesema Mheshimiwa Seif.



Hayo yameibuka  baada ya  diwani wa kata ya Mwera Mheshimiwa JAMHURI GOGO kuwaomba viongozi wa kata nyingine kuchangia ujenzi wa kituo hicho ambacho kitawasaidia wananchi wa maeneo tofauti hasa kuanzia aneo la Bweni hadi Mkalamo.

“Kituo cha afya cha Mwera, sasa kinataka kiboreshwe zaidi kwa nia nzuri tu kwa maslahi mapana ya wana Pangani, wanafanyaje sasa katika kutoa msaada hususani katika michango mbalimbali yaani jambo lolote ambalo litaonekana lina maslahi kwa wanapangani hususani katika kujenga kituo chetu cha afya kile kinatugusa sisi.” Alisema Mheshimiwa Gogo.

Katika kutoa ufafanuzi juu ya suala hilo Mkurugenzi mtendaji  wa halmashauri ya wilaya hiyo Bwana SABAS DAMIAN CHAMBASI amesema  kilichoelezwa na diwani Gogo ni jitihada za halmashauri na vijiji kwani serikali kuu tayari imekwishatoa shilingi milioni 400 za ujenzi wa kituo hicho.

“Fedha zililetwa milioni mia nne na serikali kuu na hiyo ni sehemu ya jitihadi zinazotakiwa kuchangia maendeleo ya ujenzi wa kituo cha afya, sasa mpango wetu kama anavyoeeleza Mheshimiwa diwani wa kata ya Mwera kwamba sasa anataka mchango wa jitihada kutoka halmashauri , kutoka kwenye vijiji na kwa watu binafsi.” Amesema Bwana Sabas.



Pamoja na hayo aliyekuwa diwani mteule wa kata ya Madanga  Bwana ATHUMANI TUNUTU kupitia chama cha mapinduzi CCM ameapishwa kuwa diwani rasmi wa kata hiyo  na kukabidhiwa vitendea kazi ili kuanza kuwatumikia wananchi wa kata hiyo baada ya kumalizika kwa  uchaguzi mdogo uliofanyika Februali 17 mwaka huu.

No comments

Powered by Blogger.