KAMATI YA SHULE YA MSINGI KIJIJI CHA SANGE (W) PANGANI YAAHIDI MSHIKAMANO



 (Bwana Donald Katanji akifanyiwa mahojiano na mwandishi wa Pangani Fm Mohammed Hammie)

Kamati ya Shule ya Msingi kijiji cha Sange Wilayani Pangani kwa kushirikiana na wazazi imeahidi kuweka mshikamano katika kupambana na changamoto ya suala la ukatili kwa watoto ambalo limejitokeza wakati wa mafunzo ya Minna dada yaliyodumu kwa muda wa siku tatu katika kijijini hapo.

Akizungumza wakati wa hitimisho la mafunzo hayo mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambae pia ni katibu wa kitongoji cha Sange Kuu Bwana DOLDAN KATANJI, amesema kuwa suala la kutokomeza ukatili kwa watoto linapaswa kuwa na mshikamano ili kumnusuru mtoto katika madhila hayo.

“Ni kwamba tushirikiane pamoja kuanzia wazazi, kamati, sisi viongozi wa vitongoji na vijiji, tushikamane na wadau mbalimbali ili tuweze kumuondoa mtoto huyu katika madjila ya kufanyiwa vitendo vya ukatili ili sasa ajitambue kwamba yeye ni nani” Amesema Bwana Katanji.

 (Mjumbe wa kamati ya shule ya msingi ya kijiji cha Sange Bi NINJAMA  BAKARI akilia baada ya kushindwa kuvumilia taarifa ya utafiti wa ukatili kwa watoto iliyotolewa wakati wa mafunzo hayo)


Kwa upande wake mjumbe mwengine wa kamati hiyo  Bi NINJAMA  BAKARI  ameonesha kusikitishwa na taarifa ya ukatili kwa watoto iliyotokana na utafiti uliofanywa na kundi la Banja Basi  baada ya kuzungumza na watoto wa eneo hilo kupitia mfumo salama wa kuripoti matukio ya kikatili, ambapo aliitaka kamati hiyo kutambua na kutekeleza majukumu yao.

“Toka semina yetu ianze mpaka hivi leo nimejifunza mengi, na nikianza kuyasema yanayoniuma ndani ya nafsi sitaweza kuyamaliza, kubwa zaidi ambalo limeniumiza ni hii orodha ambayo ameitoa mkufunzi! Watoto wengi wameathirika na mimi ni mzazi, pamoja na kwamba wa kwangu hajatajwa siwezi sema kama yuko salama! Roho inaniuma, inaniuma vibaya, kamati hii itambue majukumu yake” Amesema Bi Ninjama.



Kwa upande wake Afisa ufuatiliaji na tathmini pamoja na utafiti kutoka shirika la Uzikwasa  Bwana KENNEDY MASHEMA, amewaeleza wajumbe wa kamati hiyo kuwa tayari shirika hilo lina mfumo salama wa kutolea taarifa matukio ya ukatili kwa watoto, ambo huwa wanafundishwa  namna ya kutoa taarifa hizo kwa walimu na walezi wawapo shuleni.

“Ni mfano ambao tunautumia katika kurekodi kumbukumbu za ukatili kwa wototo, na hizi kumbukumbu lazima ziwe zina mfumo rasmi, ambao kwa wale watoto 14 ambao tumefanya nao majadiliano tukapata taarifa huwa wanawakilishwa na kila darasa watoto wawili mvulana na msichanaAmesema Bwana Kennedy Mashema na kuongeza kuwa…

“Kwa hiyo wale watoto wamefundishwa namna gani ya kugundua masuala mazima ya ukatili, akikuona unamkonyeza anajua kuwa hii ni ishara ya kwenda kufanyiwa ukatili. Kwa hiyo wamefundishwa namna ya kuja kuripoti kwa mwalimu mkuu au mwalimu mlezi wa kiume (Patron) au mwalimu wa kike mlezi (Matron)” Amesema Afisa huyo ufuatiliaji na tathmini pamoja na utafiti kutoka shirika la Uzikwasa.



Kambi ya mafunzo ya Minna dada imemalizika rasmi jana kwa tamasha kubwa la sanaa kutoka kundi la BANJA BASI, huku likipambwa na onesho la vidokezo vifupi vya video yaani video spot pamoja na sinema.


No comments

Powered by Blogger.