Wasimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika November 24-2019 katika Halmashauri ya Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga, wameapishwa kiapo cha Uadilifu na kuonywa kujihusisha na masuala ya ushabiki wa vyama vya kisiasa.
Hayo yamejiri katika Ukumbi wa Halmashauri hiyo, ambapo wasimamizi hao pia wametakiwa wazingatie sheria, kanuni, taratibu na miongozo katika uchaguzi huo ili kuepusha malalamiko yasiyo ya lazima.
Akizungumza na wasimamizi hao ambao miongoni mwao ni watumishi wa Serikali, Bwana KARIA MAGARO ambaye ni msimamizi wa Uchaguzi Wilayani humo, amewataka wasimamizi hao kusimamia nafasi zao za utumishi bila kujihusisha na itikadi za kisiasa.
“Tukumbuke nchi yetu ni ya kidemokrasia na jukumu hili tunalolitekeleza ni jukumu la kitaifa,kikubwa tufanye kwa kuzingatia sheria,kanuni,na miongozo mbalimbali,serikali imewapa watumishi jukumu hili maana yake sisi sio wana siasa maana yake unatekeleza majukumu yako ka kufuata kanuni na taratibu.”
Kwa Upande mwingine Mkaguzi wa Polisi Inspector HARUNA HASSANI akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Polisi Wilayani Pangani, ametaja taratibu za kisheria kipindi chote cha uchaguzi, ikiwemo vurugu ambazo zitasababisha uvunjifu wa Amani.
“Kila kiongozi au mwanachama,hatatakiwa kukaa kwa nguvu kwenye kituo cha kupigia kura,kuhamasisha wanachama au wapiga kura kupiga kura zaidi ya mara moja katika kituo cha uchaguzi,kutumia lugha ya matusi kwa msimamizi wa uchaguzi,kufanya fujo au vurugu yoyote katika mkutano wa chama kingine,kuzuia wafuasi wa chama kingine kuhudhuria mkutano wa kampeni au kuwazuia kupiga kura”
Naye Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilayani Pangani Bwana ANDREW PAUL MUSHI, amezungumzia Madhara ya Rushwa wakati wa uchaguzi ikiwemo kukosa viongozi wenye uwezo wa kuwaongoza wananchi.
“Miongoni mwa makosa ya rushwa ni kama vile kutoa zawadi au mkopo ili upate uteuzi,au kufanya makubaliano yoyote ya kutoa zawadi kwa ajili ya kupata nafasi ya kuchaguliwa,kwa upande wa madhara ya rushwa ni pamoja na rushwa huondoa uhuru wa mpiga kura,wagombea wenye vipaji na uwezo hukosa nafasi ya kuongoza kutokana na kukosa fedha,pia viongozi walichaguliwa kwa njia ya rushwa itapelekea baadae kuwa mbadhirifu kwa sababu kama yeye amepita kwa njia hiyo itakuwa ni vigumu kwake kupinga rushwa hivyo hayo yote yakibainishwa mtu huyo anaweza kufikishwa mahakamani.”
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajiwa kufanyika November 24 mwaka huu nchi nzima, ambapo zoezi la kuchukua fomu kwa wagombea litaanzia Tarehe 29 mwezi wa kumi na mwisho wa kurudisha fomu ni Tarehe 4 mwezi wa 11 mwaka huu, ambapo uteuzi wa wagombea utafanyika Tarehe 5 mwezi wa 11-2019, huku kampeni zikitarajiwa kufanyika siku 7 kabla ya uchaguzi kuanzia Tarehe 17 November na kampeni hizo zitafikia tamati Tarehe 23 November, na siku itakayofuata itakuwa ni zoezi la upigaji kura.
No comments