WANANCHI WA KATA YA BWENI WILAYANI PANGANI WAMLALAMIKIA MTENDAJI WAO
Wananchi wa Kata ya Bweni wilayani Pangani
wamelalamikia utendaji kazi wa Afisa mtendaji wa Kata hiyo kutokana na
walichokiita kutofuata utaratibu na maadili ya utumishi wake.
Wakizungumza wakati wa Mkutano mkuu wa dharura ambao
umefanyika mbele ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo katika kijiji cha
Bweni, wananchi hao wamesema mtendaji huyo amekuwa akifanya mambo mbalimbali
yasiyofaa ikiwemo kutoza pesa za barua, kutoa siri za serikali pamoja na kupoteza
baadhi ya nyaraka za serikali, huku wakimuomba mkurugenzi huyo kumuondoa katika
kata hiyo.
Awali katika mkutano huo Diwani wa Kata ya Bweni
Bwana Kassim Saidi Omari ameelezea kusikitishwa na kitendo cha mwananchi mmoja
kuteka eneo la zahanati na shule ya msingi Kikokwe, suala ambalo halijapatiwa
ufumbuzi kutokana na kukosa ushirikiano na mtendaji huyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya
ya Pangani Ndugu Sabas Damiani Chambasi, amesema masuala yote atakwenda
kuyafanyia kazi kulingana na taratibu na sheria za kiutumishi, huku akiwaagiza
baadhi ya viongozi wa kata na kijiji hicho kuhakikisha wataalamu wanaofanya
kazi katika kata yao wanawajibika ipasavyo ili kuleta Maendeleo.
Hayo yamejiri katika Mkutano maalumu wa kujadili
mgogoro wa uvamizi wa eneo la shule ya msingi na zahanati ya kikokwe kijiji cha
Bweni, huku kikihudhuriwa na Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Pangani.
No comments