ZIFAHAMU SIKU 1000 MUHIMU KWA AFYA YA MTOTO
Mwarobaini
na mustakabali bora wa mtoto katika dunia, unatokana na jamii kuwekeza zaidi
katika siku elfu moja (1000) za
mtoto, kuanzia siku ya kwanza wazazi wanakutana kimwili, kipindi cha kulea
ujauzito na baada ya kujifungua.
Hayo yamesemwa katika kipindi cha
ASUBUHI YA LEO kinachorushwa na kituo hiki na Afisa Lishe kutoka taasisi ya
chakula na lishe nchini Tanzania chini ya Wizara ya Afya kutoka Dar es Salaam Bi
DEBORA CHARWE, na kuongeza kuwa siku elfu moja ni muhimu kwa ukuaji bora wa
mtoto, na ndio mustakabali wa maisha yake yote.
“Siku elfu moja za mtoto zinaweza zikawa
ni siku muhimu kwenye maisha yake katika hatua yoyote ile, lakini siku elfu
moja zinazozungumziwa katika kipengele cha lishe tunamaanisha tangu mimba
inapotungwa mpaka mimba inakuwa na mama anajifungua, na yule mtoto atapotimiza
miaka miwili yaani miezi ishirini na nne” Amesema Bi Debora na kuongeza kwamba…
“Katika siku hizi elfu moja, usipofanya
mambo yanayotakiwa kwa ajili ya yule mtoto wako, basi itakuwa umemharibu mtoto
kabisa”
Bi Debora ameongeza kuwa “Yapo mambo ya
kufanya, yapo mambo ya kutekeleza ili tuweze kupata kizazi ambacho ni imara na
chenye akili, ni kizazi ambacho kitaweza kufanya maamuzi na vitu vikubwa sana
na kuongeza uchumi katika nchi yetu na pia kuongeza uzalishaji” Amesema.
Aidha Bi DEBORA amesisitiza kuwa katika
kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito, ni muhimu katika kumjenga mtoto
awapo tumboni hasa kwa kuzingatia suala la lishe, hivyo ametoa wito kwa
wanawake pindi wanapokuwa wajawazito kuzingatia suala la lishe bila kujali hali
zao za kutotamani baadhi ya vyakula.
“Hiyo miezi ambayo kuna vurugu za
kutapika, sijui kufanyaje, hiyo ndio miezi ya muhimu sana, na watoto wengi
wameharikia hapo, unasikia siku hizi kuna migongo wazi, vichwa vikubwa ni
wakati ule virutubishi hapo vilikosekana wakati huo” Amesema Bi Debora na
kuongeza kuwa…
“Kwahiyo sasa nina wahamasisha wanawake
wenzangu, ninajua zile adha wanazozipata wakati huo, lakini ninaendelea
kuwahamasisha kwamba ukitapika, amka omba bakuli jingine kula, jikaze fikiria
maisha ya yule aliyetumboni” Amesema kwa msisitizo.
Amemalizia
kwa kusema kuwa kukamilika kwa yote yaliyomuhimu kwa mwanamke kabla, wakati na
baada ya kujifungua, mwanaume ndio msingi mkubwa wa kufanikisha hayo, hivyo
ameshauri kinababa kuwa karibu na wenzao, katika kuhakikisha usalama na ukuaji
bora wa mtoto.
“Mwanaume ni mtu mmoja muhimu sana katika
yote niliyosema, bila mwanaume kusisitiza, bila mwanaume kuvileta kwa mfano
nimesema ulaji wa nyama, nani anayenunua nyama ni baba ndio eeh! Muhimize yaani
aone wewe kama ulivyoiweka ile mimba ndio mdau mkubwa sana katika ile mimba
wewe na mama” Amesema Bi Debora Charwe na kuongeza kuwa…
“Bibi, wifi na shangazi wao wanafata
baadae wakati wewe baba labda umekwenda shambani ndio wanakaa na yule mjamzito
wanamsaidia” Amesema.
Wataalam wa lishe
wanasema, siku 1000 ni kipindi ambacho kinaweza kujenga jamii ya badaye kuwa
yenye afya nzuri imara na yenye mafanikio.
No comments