AJERUHIWA NA PANGA WAKATI AKIIBA MIHIGO HUKO MADANGA



Kijana mmoja  mkazi wa kijiji cha Madanga Wilayani Pangani amejeruhiwa kwa  kukatwa na Panga katika mkono wake wa kulia baada ya  kukutwa aking’oa Mihogo shambani kwa Bwana MWINYIHAJI KARAFUU bila  idhini  ya mmiliki wa shamba hilo.

Akithibitisha kutokea  kwa tukio hilo  kamanda  wa polisi  wilaya ya Pangani Bi CHRISTINA MUSYANI amesema kuwa  mnamo  tarehe 5  mwezi huu wa pili  majira ya saa tisa Alasiri Bwana MDABIDA CHAMBEGA mkazi wa kijiji cha Madanga, alijeruhiwa baada ya kukutwa  akiiba Mihogo shambani kwa Bwana KARAFUU yenye thamani ya shilingi elfu sita.

“Ni kweli taarifa hizo zipo, ambapo tukio hilo lilitokea tarehe 5 February 2018 majira ya saa Tisa na robo hivi Alasiri, kwamba ndugu Mdabida Chambega (30) ambaye anaishi Madanga alijeruhiwa kwa kukatwa katika mkono wake wa kulia kwa kutumia Panga na ndugu Mwinyihaji Karafuu”. Amesema Kamanda huyo wa Polisi Pangani na kuongeza kuwa.

“Huyu Mdabida alikuwa katika shamba la Mihogo la Bwana Mwinyihaji alikuwa akivuna bila kuruhusiwa ina maana alikuwa akiiba, hivyo ndugu Mwinyihaji alipogundua kuna mtu anavuna katika shamba lake akamshambulia kwa Panga, lakini Mihogo ambayo wakati huo ameshaing’oa ilikuwa na thamani ya shilingi elfu sita”.

Aidha Bi Musyani amewataka wananchi kuwa waaangalifu na kutii sheria za nchi zilizowekwa, pamoja na kuacha kujichukulia sheria mkononi.

“Huyo Bwana Mdabida alikutwa anaiba Mihogo isiyo ya kwake, tunasisitizana kila siku kutokuchukua sheria mkononi, tuwe waangalifu, kwa sababu unakuta inaibua hiyo ya kujeruhi wakati tulikuwa na kesi ya msingi ya wizi. Sasa hapo naendelea kusisistiza jamii ya Pangani kuwa waangalifu katika haya wasichukue sheria mkononi”. Amesema Kamanda Musyani.

Katika hatua nyingine Kamanda Musyani amewataka wananchi kufanya kazi na kutumia rasilimali ardhi katika shughuli za kilimo, na kuacha vitendo vya wizi kwani vinarudisha nyuma maendeleo.

No comments

Powered by Blogger.