ZIFAHAMU SIKU 1000 MUHIMU KWA AFYA YA MTOTO



Mwarobaini na mustakabali bora wa mtoto katika dunia, unatokana na jamii kuwekeza zaidi katika siku elfu moja (1000) za mtoto, kuanzia siku ya kwanza wazazi wanakutana kimwili, kipindi cha kulea ujauzito na baada ya kujifungua.

Hayo yamesemwa katika kipindi cha ASUBUHI YA LEO kinachorushwa na kituo hiki na Afisa Lishe kutoka taasisi ya chakula na lishe nchini Tanzania chini ya Wizara ya Afya kutoka Dar es Salaam Bi DEBORA CHARWE, na kuongeza kuwa siku elfu moja ni muhimu kwa ukuaji bora wa mtoto, na ndio mustakabali wa maisha yake yote.

“Siku elfu moja za mtoto zinaweza zikawa ni siku muhimu kwenye maisha yake katika hatua yoyote ile, lakini siku elfu moja zinazozungumziwa katika kipengele cha lishe tunamaanisha tangu mimba inapotungwa mpaka mimba inakuwa na mama anajifungua, na yule mtoto atapotimiza miaka miwili yaani miezi ishirini na nne” Amesema Bi Debora na kuongeza kwamba…

“Katika siku hizi elfu moja, usipofanya mambo yanayotakiwa kwa ajili ya yule mtoto wako, basi itakuwa umemharibu mtoto kabisa”



Bi Debora ameongeza kuwa “Yapo mambo ya kufanya, yapo mambo ya kutekeleza ili tuweze kupata kizazi ambacho ni imara na chenye akili, ni kizazi ambacho kitaweza kufanya maamuzi na vitu vikubwa sana na kuongeza uchumi katika nchi yetu na pia kuongeza uzalishaji” Amesema.

Aidha Bi DEBORA amesisitiza kuwa katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito, ni muhimu katika kumjenga mtoto awapo tumboni hasa kwa kuzingatia suala la lishe, hivyo ametoa wito kwa wanawake pindi wanapokuwa wajawazito kuzingatia suala la lishe bila kujali hali zao za kutotamani baadhi ya vyakula.

“Hiyo miezi ambayo kuna vurugu za kutapika, sijui kufanyaje, hiyo ndio miezi ya muhimu sana, na watoto wengi wameharikia hapo, unasikia siku hizi kuna migongo wazi, vichwa vikubwa ni wakati ule virutubishi hapo vilikosekana wakati huo” Amesema Bi Debora na kuongeza kuwa…
“Kwahiyo sasa nina wahamasisha wanawake wenzangu, ninajua zile adha wanazozipata wakati huo, lakini ninaendelea kuwahamasisha kwamba ukitapika, amka omba bakuli jingine kula, jikaze fikiria maisha ya yule aliyetumboni” Amesema kwa msisitizo.



Amemalizia kwa kusema kuwa kukamilika kwa yote yaliyomuhimu kwa mwanamke kabla, wakati na baada ya kujifungua, mwanaume ndio msingi mkubwa wa kufanikisha hayo, hivyo ameshauri kinababa kuwa karibu na wenzao, katika kuhakikisha usalama na ukuaji bora wa mtoto.

“Mwanaume ni mtu mmoja muhimu sana katika yote niliyosema, bila mwanaume kusisitiza, bila mwanaume kuvileta kwa mfano nimesema ulaji wa nyama, nani anayenunua nyama ni baba ndio eeh! Muhimize yaani aone wewe kama ulivyoiweka ile mimba ndio mdau mkubwa sana katika ile mimba wewe na mama” Amesema Bi Debora Charwe na kuongeza kuwa…

“Bibi, wifi na shangazi wao wanafata baadae wakati wewe baba labda umekwenda shambani ndio wanakaa na yule mjamzito wanamsaidia” Amesema.

Wataalam wa lishe wanasema, siku 1000 ni kipindi ambacho kinaweza kujenga jamii ya badaye kuwa yenye afya nzuri imara na yenye mafanikio.

No comments

Powered by Blogger.