MAHAKAMA PANGANI YAADHIMISHA SIKU YA SHERIA NCHINI



Mahakama wilayani Pangani kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wameungana katika kuadhimisha siku ya sheria nchini iliyokuwa imebeba kauli mbiu isemayo ‘Matumizi Ya Tehema Katika Utoaji Haki Kwa Wakati,’ shughuli iliyofanyika katika ukumbi wa ofisi hizo zilizopo Pangani Mjini.

Akizungumzia kauli mbiu hiyo Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Pangani, Bi Crisencia Kisongo amesema kuwa, mfumo wa Tehama utasaidia kuhifadhi taarifa za mashauri za kimahakama  na utarahisisha upatikanaji wa majalada huku ukisaidia upatikanaji wa malalamiko kwa wateja.

‘'Mahakama ndio chombo pekee nchini ambacho kina jukumu la kutoa haki , Mahakama kama ilivyo vyombo vingine au mihimili mingine haiko nyuma kwenye matumizi ya Tehama, tayari imeshaanza na tayari inaendelea na matumizi ya hiyo teknolojia ya habari na mawasiliano’’ Amesema Bi Crisencia.



Bi Crisensia pia amewataka wananchi wilayani Pangani kutosita kuuliza kwa wataalamu wa sheria juu ya maswala mbali mbali ya kisheria.

‘’Tuseme tu watumishi wote wa kimahakama, mahakimu na viongozi wote wapo tayari kuendelea kutoa elimu kuhusiana na shughuli mbali mbali zinazofanywa na mahakama wakati wote tunawakaribisha” Amsemema Bi Kisongo.



Kwa upande wa wananchi waliojitokeza katika kilele hicho hawakusita kutoa maoni yao kwa vyombo vya sheria wilayani humo huku wakiviasa kutenda haki.
‘’Siku ya sheria leo nashukuru imekwenda vizuri na kuna baadhi ya vipengele ambavyo tumejaribu kuhamasishwa au kutusaidia sisi ambao ni watu wa chini na kwamba mambo ya kisheria tulikuwa tunayaona ni mageni na tunaimba mahakama iwe inatenda haki’’ Amesema mmoja wa wananchi.
 


Mgeni Rasmi wa Maadhimisho hayo ya sheria wilayani Pangani ni Bwana Peter Mabuga ambaye ni katibu tawala wilayani Pangani, amewataka wananchi kuchukua hatua kwa maafisa wa Mahakama wanaowaomba rushwa pamoja na kuwaasa watumishi wa Mahakama kutenda haki.

‘’Tusiishie kulalamika, chukueni hatua dhidi ya maofisa wa mahakama ambao wanakiuka maadili ya kazi zao wanaojihusisha na vitendo vya rushwa badala ya kulalamika kimnywa kimnywa tu.’’ Amesema Mabuga.

Maadhimisho ya kilele cha siku ya sheria nchini Tanzania hufanyika kila mwaka mwanzoni mwa mwezi wa pili, ambapo kwa mwaka huu yaliobeba kauli mbiu isemayo MATUMIZI YA TEHEMA KATIKA UTOAJI HAKI KWA WAKATI.


No comments

Powered by Blogger.