ANASURIKA KIFO BAADA YA KUNYWA SUMU YA PANYA


 Kijana mmoja mkazi wa Kitongoji cha Kimang’a B Wilayani Pangani ambaye jina lake limehifadhiwa, amenusurika kufa baada jaribio la kutaka kujiua kwa kunywa sumu ya Panya akidai kuwa maisha ni magumu.

Akizungumza na Pangani Fm Kamanda wa Jeshi la Polisi Wilayani humo Bi Christina Musyani, amethibitisha tukio hilo na kusema kuwa baada ya kupata taarifa kwa wasamaria wema walifuatilia  suala hilo na baadae kugundua  kuwa ni kweli ambapo haraka mtu huyo alikimbizwa kituo cha Afya ili kuokoa maisha yake.

“Taarifa hii ni ya kweli sisi tumeithibitisha kw asababu tulipata taarifa tarehe 11 mwezi huu wa pili majira ya alfajiri, kwamba kuna kijana katika kitongoji cha Kimang’a B alikuwa amejaribu kujiua usiku wa tarehe 10 majira ya saa tano na nusu usiku akiwa ndani ya nyumba yake” Amesema kamanda Musyani na kuongeza kuwa….

“Alijaribu kujiua kwa kunywa sumu ya Panya lakini tunashukuru Mungu kwamba hakuweza kufariki, ndugu yake aliweza kumgundua mapema na kutoa hizo taarifa na akakimbizwa katika kituo cha afya akapata huduma”.

Aidha Kamanda Musyani amesema kuwa mtu yoyote anae jaribu kudhuru mwili wa mtu mwingine ama mwili wake, ni kosa kisheria na hivyo kutokana na hilo kijana huyo anashtakiwa na atapelekwa Mahakamani, huku akiwahimiza vijana kufanya kazi kwa bidii ili waweze kujikimu kimaisha.

 “Mimi nitoe wito kwa vijana na rika lote kujiua sio suluhisho, tujibidiishe katika kazi na tufanye kazi sahihi itayotambulika yaani halali ili upate kipato uweze kujikimu, mbona tuna ardhi ya kutosha hebu tuitumie kwa maslahi mapana ya maisha yetu”. Amesisitiza kamanda huyo   
 


No comments

Powered by Blogger.