WANANCHI PANGANI WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA MAHAKAMA ILI KUPATA HAKI ZAO



Wananchi wilayani Pangani na nje ya Wilaya hiyo wametakiwa kushirikiana na Mahakama ili kurahisisha kumaliza mashauri kwa haraka kwa mujibu wa sheria ili haki iweze kupatikana kwa wakati.

Akizungumza wakati wa kipindi cha Asubuhi ya leo kinachorushwa na Pangani FM Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mwera pamoja na eneo la Mkalamo Bwana Antony Clement Hamza amesema kuwa wananchi wanatakiwa kutimiza yale wanayoamriwa kwa kutoa ushirikiano ili kuirahisishia Mahakama utekelezaji wake kwani wapo tayari kuwasikiliza.

‘Tupo tayari kuwasikiliza watimize yale ambayo wanaamriwa kwa ajili ya kufikia zile haki zao ambazo wanataka kuzipata na hiyo itasaidia ule utaratibu wetu wa kusikiliza maashauri kwa wakati na kutoa maamuzi kwa haraka, wasipotoa ushirikiano kwa kutimiza yalioamriwa na maelekezo yaliyoamriwa basi yataweka mkwamo kwa kufikia malengo kwetu sisi kwa kumaliza mashauri haraka na wao kupata haki kwa wakati” Amesema Bwana Hamza.



Kwa upande wake Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo mjini Pangani Bwana PAUL MAGESA  amewataka wananchi kufika katika Mahakama ili kujifunza sheria mbalimbali na kufahamu sehemu ya kuweza kupata haki zao za kimsingi.

“Kwanza waione Mahakama ni chombo chao kwa hiyo wafike Mahakamani si lazima wasubiri siku za elimu ya sheria, vile vile wapende kujifahamisha zaidi taratibu, zipo taasisi mbalimbali zinazotoa elimu ya msaada wa sheria lakini zaidi kabisa ni kuwa na uelewa kwamba nikiwa na haki yangu naipata wapi kwa maana ni jambo la kwenda Mahakamani usipoteze muda kwa kupita katika ofisi nyingine ambazo hazitakupa majibu kwenye jambo lako nenda kwenye chombo husika uweze kupata haki yako” Amesema Bwana Magesa



Katika kuelekea juma la sheria nchini Tanzania ambalo lilianza Januari 27 mwaka huu, Hakimu Antony Hamza amesema tayari wameanza kutoa elimu kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ikiwemo sokoni mjini Pangani pamoja na Mahakamani kuhusu sheria mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wa sheria ikiwemo jeshi la Polisi, TAKUKURU na wasaidiazi wa kisheria PACOPA.

Hayo yamekuja  wakati nchi ya Tanzania ikielekea kuadhimisha siku ya sheria nchini itakayofanyika tarehe 1/2/2018.

No comments

Powered by Blogger.