WADAU PANGANI WAKOMAA NA ELIMU!
Wadau mbali mbali wa elimu wilayani
Pangani Mkoani Tanga wamesema wapo tayari kufikisha kwenye Jamii kile ambacho
wamekipata kwa muda wa siku tatu mfululizo katika mafunzo ya Minna Dada yaliyomalizika
mwishoni mwa wiki iliyopita katika kijiji cha Msaraza, ambapo mbali na mambo
mengine suala la elimu lilijadiliwa kwa mapana zaidi.
Wakizungumza siku ya mwisho ya Mafunzo
hayo wadau hao wamesema watahakikisha wanasimamia vyema maendeleo ya watoto
shuleni, pamoja na kutumia Mafunzo hayo kujitoa katika mikwamo ambayo ilikuwa inawazuia
kupiga hatua kwenye masuala ya maendeleo.
“Kwa sababu ilikuwa wengine ufahamu wetu
ni mdogo na mpaka sasa hivi tumeelewa na elimu hii tutaipeleka kwa wenzetu na
tutahakikisha wanaelewa na wanabadilika kama tulivyobadilika sisi, ili wao na
sisi kwa kushirikiana tusongeshe mbele hili gurudumu la maendeleo”. Amesema
mmoja ya wajumbe walioshiriki mafunzo hayo.
Kwa upande mwingine wanakamati hao
wamesema wameweza kujitafakari na kuona makosa binafsi waliyowahi kuyafanya
suala ambalo ni gumu, ila kupitia mafunzo hayo imekuwa rahisi kufanya hivyo,
huku wakitoa shukrani zao za dhati kwa shirika la UZIKWASA kwa mafunzo ambayo
yataendeleza kijiji chao.
“Somo
la kusema kuwa tujimulike wenyewe, hata katika dini ya kiislam tumeambiwa kuwa “sema kweli ijapokuwa inauma” ina maana
mtu akubali kulitoa lake la moyoni ambalo linamkereketa hata kama ni uzembe
aliusababisha yeye, akubali na akiri kwamba hili lilikwama kwa sababu yake
yeye”. Amesema mmoja wa washiriki.
Mafunzo ya kambi ya Minna Dada
yanatolewa na shirika la UZIKWASA, ambayo yana lengo la kujengeana uwezo na
kuwezeshana wadau wa maendeleo na kamati ya shule za msingi namna ya kutumia
mbinu wezeshi kutatua changamoto za wanafunzi shuleni na nje ya shule ili
wafikie ndoto zao, mafunzo hayo pia yameshirikisha baadhi ya wataalamu kutoka
halmashauri ya wilaya ya Pangani.
No comments