TATIZO LA MATUNDU YA VYOO SHULE YA MSINGI PANGANI LAWAKUTANISHA WADAU
Katika kukabiliana na tatizo la upungufu wa matundu
ya vyoo kwenye shule ya msingi Pangani uongozi wa kata ya Pangani Magharibi umekutana
na wadau wa maendeleo ili kujadili namna ya kutatua tatizo hilo.
Akisoma taarifa
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Mwalimu Hamisi Mohamed amewaeleza wadau hao
kuwa tatizo la upungufu wa matundu ya vyoo shuleni hapo lichukuliwe kuwa la
dharura kwani choo kilichopo chenye matundu kumi na nne yaani wasichana matundu
saba na wavulana matundu saba, kimekuwa kibovu na kina nyufa jambo ambalo
linaweza kupelekea madhara.
“Ndugu wadau wa elimu, shule ya msingi Pangani choo
kilichopo chenye matundu 14 chenyewe kimekuwa kibovu na kina nyufa kubwa kitu
ambacho kinaweza kusababisha hatari hapo baadaye, lakini pia tumepata msaada wa
choo chenye matundu sita kutoka Islamic Help lakini mpaka sasa hakijakamilika,
ziko chemba ambazo hazijafungwa pia mtiririko wa maji bado haupo”. Amesema
Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Pangani.
Pamoja na kuelezea makubaliano ya kikao hicho
Mwenyekiti wa Maendeleo ya kata ambaye ni Diwani wa kata hiyo John Semkande,
amesema wamewashirikisha wadau ili kuona namna ya kutatua changamoto hizo.
“Kwahiyo tumeamua kuwaita
wadau leo kuwashirikisha ili kuona ni namna gani kama jamii tunaweza tukatatua
ile changamoto ya matundu 14 yale ili kuweza kuvijenga upya, tumekubaliana
tumshirikishe afisa ujenzi ili afanye tathmini ili tujue gharama ni kiasi gani
halafu tutawaambia wadau, lakini baadae tutawashirikisha wananchi kupitia vikao
vyetu”. Amesema Diwani wa kata ya
Pangani Magharibi John Semkhande.
Wilaya ya Pangani iliyopo Mkoani Tanga inakabiliwa
na upungufu wa Matundu ya vyoo katika shule mbalimbali, huku Shule ya msingi
Pangani pekee ikiwa na upungufu wa matundu ya vyoo 53.
No comments