Wananchi waishio wilayani Pangani mkoani Tanga wametakiwa kufuata kanuni za usafi ili kuepukana na ugonjwa hatari wa kipindupindu pamoja na maradhi yanayosababishwa na uchafu wa maji.
Wito huo umetolewa na Afisa Afya wilaya ya Pangani Bwana MOHAMED NYATI wakati alipotembelewa na Pangani fm ambapo amesema wananchi wanapaswa kutimiza masharti ya kiafya ikiwa ni pamoja na kutibu maji ya kunywa ili kuepukana na ugonjwa huo.
Akitoa taarifa ya hali ya ugonjwa wa kipindupindu ilivyo sasa wilayani humo Bwana NYATI amesema kuwa hivi sasa wilaya hiyo haina mgonjwa wa kipindupindu tangu aripoti mgonjwa wa mwisho na tayari wagonjwa wote wamesharuhusiwa.
Aidha Bwana NYATI amewataka wazazi kuwa makini katika kuwaangalia watoto wao ili wasinywe maji yasiyosafi na salama kwani mtoto anapopata maradhi hayo ni rahisi kupungukiwa na maji mwilini na pia amewataka wananchi wanaouza vyakula mashuleni viwe salama.
Hayo yamekuja kufuatia hivi karibuni wilaya ya Pangani kuripotiwa uwepo wa ugonjwa wa kipindupindu ambapo kwa sasa hakuna mgonjwa yeyote katika kambi zote wilayani humo. Hivyo kila mwananchi kutakiwa kutimiza kanuni za usafi.
No comments