DC PANGANI 'KULA SAHANI MOJA' NA WAWEKEZAJI WASIO NA TIJA
Mkuu wa Wilaya ya Pangani Bi Zainab Abdallah Issa
amesema kuwa umefika wakati sasa wawekezaji wote wasiona tija Wilayani Pangani
kutovumiliwa kufuatia uwekezaji wao kutokuwa na manufaa ya kuleta Maendeleo wilayani
humo.
Akizungumza na Pangani FM hivi karibuni Mkuu huyo wa
Wilaya amesema kuwa, umefika wakati wa kuwaondoa wawekezaji wote wanaoshindwa
kuchangia katika miradi ya kimaendeleo, ilhali wao wananufaika kwa kiasi kubwa
na rasilimali zilizotunzwa vizuri na wanapangani wenyewe.
“Nachukuwa
nafasi hii pia nimuombe Mkurugenzi na wataalamu wake, ifike mahali msikae kimywa,
haya mambo mengine hayavumiliki hii ni wilaya yetu, kuna baadhi ya wawekezaji
wilayani kwetu hawana tija, hivyo wanapaswa kufahamu kwamba sisi ndio serikali
na sisi ndio dola hapa wilayani hatumuogopi mtu, kuna watu wanavimba huko
mitaani wakiamini wao wana pesa na wana miradi mikubwa ya uwekezaji hapa
wilayani Pangani lakini kwetu hawana tija yeyote” Amesema Bi Zainabu.
Pamoja na hayo Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa
mpango alionao ni kuhakikisha anakutana na wawekezaji wote waliopo wilayani
humo kwenye kikao maalum, huku akikemea kitendo cha wawekezaji pindi wanapoitwa
kutuma wawakilishi wao.
“Kwa hiyo na mimi natuma salamu zangu kwa wawekezaji
wa hapa wilayani Pangani, nitakuwa na kikao na wawekezaji wote na kuna desturi
kuna mtu akisikia kuna kikao anatuma muwakilishi mtu ana tuma hadi dereva wake aje
kuwakilisha kwenye kikao, hebu fikiria dereva kweli? Sasa ifike mahala tufunge
ofisi zao na waje kwenye kikao ili wajuwe serikali ipo, tunaenda nao
kiubinadamu na kistaarabu lakini tunashindwa kuheshimiana basi tuchukuwe hatua
kali, leo tunashindwa kujenga hata kituo cha Polisi tunaomba msaada nje wakati
wapo wawekezaji wa hapa ndani na wanatumia rasilimali za wilaya hii lakini
hawajaona umuhimu wa kusaidia wananchi’’ Alimalizia kwa msisitizo Mkuu wa
Wilaya.
No comments