AFISA USHIRIKA, NMB PANGANI WAKUTANA NA WANACHAMA WA SACCOS




Suala la elimu ya ushirika na usimamizi wa fedha kwa wajumbe wa bodi na wanachama wa chama cha ushirika Mwera na Sakura Estate wilayani Pangani, limeonekana kuwa chini hali iliyosababisha baadhi ya wanachama hao kushindwa kufanya kazi zao kulingana na taratibu za ushirika.



Hayo yameelezwa na Afisa ushirika wilayani Pangani Bwana Julius Chagama katika mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika katika kijiji cha Mwera kwa kuwashirikisha benki ya NMB tawi la Pangani, ambapo amesisitiza kuwa elimu ya ushirika  na usimamizi ni muhimu kwani ndiyo inayomsaidia mwanachama na mjumbe wa bodi katika kuweka akiba.

“Ndio maana bado tunasisitiza kwamba elimu ya ushirika ni muhimu kwa mujibu wa sheria, na wakati wowote ukiangalia sheria zetu hata ukianzia huko nyuma zilikuwa zinatenga asilimia ishirini na tano ya ziada inayopatikana kwa mwaka kwaajili ya elimu, elimu haiishii kwenye mkutano mkuu tu kama wanachama naona hapa wanaelewa hivyo,  kuna elimu kwa viongozi wa bodi lakini kupitia kwenye kamati zao kama vile kamati za mikopo kamati ya usimamizi lakini pia kuna elimu ya watendaji.”Amesema Bwana Chagama.



Kwa upande wake aliyekuwa mwenyekiti wa bodi hiyo kwa awamu iliyopita  Bwana Kibaden Laurian amesema baada ya kupata elimu ya ushirika,  baadhi ya watu wamepata muamko na kujua umuhimu wa kuweka akiba tofauti na awali.

“Wakati tunaanza wengi walikuwa hawajui ushirika lakini baada ya kupata sasa semina kutoka kwa mrajisi wa wilaya Bwana Chagama baadhi wameweza kupata mwamko na kuendelea kijiunga zaidi na kuelewa umuhimu wa kuweka akiba, kwa sababu wengi wamekuwa na mawazo kwamba kipato wanachokipata ni kidogo kwa hiyo hana uwezo wa kuweka pesa nyingine  kwenye mfuko wa saccos ili aweze kukopa ili aweze kupata pesa ya kutosha ili aweze kufanya shughuli nyingine, kwa hiyo inaonyesha kwamba elimu sasa kadri tunavyoendelea kipindi tulichokuwepo tumejitahidi kadri ya uwezo wetu mimi mwenyekiti pamoja na bodi yangu kwa ujumla” Amesema Bwana Kibaden.



Abel Chitojo ni meneja wa tawi la NMB Pangani ambaye ni mgeni rasmi kwenye mkutano huo amesema kuwa kutokana na wanachama walio wengi kutokuwa na uelewa juu ya elimu ya kifedha  wataendelea kutoa elimu hiyo na pia kuendeleza ushirikiano baina yao.

“Tutaendeleza ushirikiano na saccos ya Mwera na Sakura Estate kwani ni wateja wetu, pia kuendelea kuwapatia elimu ya kifedha hasa wanachama wake wa Mwera ambao mnajua wengi ni wafanyakazi na vibarua wadogo wadogo, kwa ajili ya kuweza kupata ule uelewa wa fedha, unajua kuna watu wanapata fedha lakini matumizi ni kama vile akipata mshahara wote unaisia kwenye chakula tu, pia kuweza kuweka na kukopa, jinsi gani unaweza kupata faida”Amesema Bwana Abel 



Nao wanachama waliojiunga na chama hicho wameelezea mafanikio waliyoyapata, huku wakiwashauri wengine kutokuwa wazito kujiunga na chama hicho.

“Wengi elimu inawaingia kutokana maendelieo madogo madogo ambayo wenzao wanaona na wanayapata, mimi mwenyewe nikiwa mwanachama na ni mjumbe naweza kusema kwamba saccos ndio imeniwezesha kwamba hadi leo najivuna nawezasema kuwa nina nyumba nzuri ya thamani, nawashauri tusiwe wazito kujiunga. Tangu tulivyoanza kwenye saccos yetu mimi nilikuwa siwezi kumiliki milioni hata mbili lakini kwa sasa namiliki zaidi ya nne” Amesema mjumbe mmoja.



Hayo yamejiri kwenye Mkutano mkuu wa chama cha ushirika Mwera wa kujadili masuala mbalimbali ya chama hicho na miongoni mwa wananachama hao ni kutoka Chama cha ushirika Mwera, Sakura, na Kigombe Estate na Tanga kilichoanza mwaka 2002.

Mbali na mkutano huo pia Benki ya NMB tawi la Pangani ilipata nafasi ya kuelimisha wanachama hao kujiunga na benki hiyo na kufanikiwa kuwafungulia akaunti baadhi ya wanachama ambao hawakuwa wanatumia huduma hiyo.


No comments

Powered by Blogger.