PANGANI NZIMA SASA KUPATA UMEME


Serikali inatarajia kukamilisha zoezi la kusambaza umeme katika vijiji  na maeneo yote wilayani Pangani ndani ya mwaka huu wa 2018 ili kuboresha maisha ya  wananchi kwa upande wa nishati kupitia mradi wa REA awamu ya tatu.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nishati Mheshimiwa Dkt. Medard Kalemani wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mivumoni wilayani humo katika ziara yake ya hivi karibuni na kusema kuwa wao kama serikali wanayo matumaini ya kuwa mradi huo utatekelezwa na kukamilishwa  ndani ya mwaka huu katika vijiji na vitongoji vyote ambavyo havina umeme wilayani Pangani japokuwa wamempa mkandarasi miezi ishirini na nne kukamilisha kazi ya kusambaza umeme wilaya nzima.

“Tumetekeleza miradi mitatu hapa Pangani kati ya vijiji  33 vilivyokuwa ndani ya wilaya yetu bado ni vijiji vitano havijapatiwa umeme, bado vitongoji vingi havijapata umeme. Msaraza ambako bado, Mtonga ambako bado, na Mtango, Bado wananchi wengi hamjaunga umeme tumemleta mkandarasi huyu tumempa miezi takribani ishirini na nne kukamilisha kazi katika wilaya nzima ya Pangani na bahati nzuri ana maeneo machache ni vijiji vitano tu na vitongoji kumi na moja tuna matumaini ndani ya mwaka huu atakamilisha mapema iwezekanavyo.” Alisema Mh.eshimiwa Kalemani.



Aidha Mheshimiwa Kalemani amesema baada ya vijiji vyote kukamilika kusambaziwa umeme mkandarasi atafanya kazi ya kurudia katika sehemu ambazo zimerukwa ili kuifanya Pangani sehemu ya mfano katika upatikanaji wa Nishati ya umeme na kuvutia wawekezaji kujenga viwanda.

Mheshimiwa Waziri Kalemani amewataka wakazi wa Pangani kuwa, mradi utakapokamilika kuitunza miundombinu yake ili iweze kudumu kwa mrefu huku akiwasisitiza kuchangamkia fursa mapema ya kuunganishiwa huduma hiyo  kwa kuwa endapo mradi ukiwa tayari gharama ya kuunganishiwa umeme itakuwa ni kubwa.

“tutunze miundombinu ya umeme inayokuja, nguzo hii ikiwekwa mtu mmoja akaikata watu zaidi ya arobaini watakosa umeme kwa mkupuo, transforma ikifungwa mtu akaiba mafuta wananchi zaidi ya mia moja watakosa umeme kwa mkupuo hivyo tutaanza kulalamika, kwahiyo niwaombe tuitunze miundombinu ili na sisi itutunze. Na wananchi ambao watachelewa muda ukaisha mradi ukapita mtaingia gharama kubwa ya kuunganisha umeme kwahiyo mimi niwaombe kabisa waheshimiwa wenyeviti wa vijiji na viongozi wengine tuwahamasishe wananchi hawa” Alisema Mheshimiwa Waziri.



Waziri huyo wa Nishati pia amewashauri wananchi wenye vyumba vichache kutoingia gharama ya kufanya wiring katika nyumba zao na badala yake watumie kifaa maalumu kinachoitwa UMETA kwa ajili ya kuepusha gharama ambapo wateja 200 wa mwanzo hadi 250 watapatiwa bure na tayari wazee watano wa kijiji cha Mivumoni wameshapatiwa vifaa hivyo bila ya malipo.

“Wananchi ambao uwezo wenu ni mdogo ambao hamjavuka hatua, kama nyumba yako ina chumba kimoja, viwili, vitatu hadi vinne msihangaike kuingia gharama ya kufunga wiring tumieni kifaa hiki kinaitwa UMETA ukiwa na chombo hiki una umeme tayari, chombo hiki kinatolewa bure kwa wateja wa mwanzo 200 hadi 250, ukiwa na chombo hiki utaunganisha umeme wake na Friji, Jiko la umeme, na utaunganisha na TV wale vijana wenzangu utaangalia mpira wa Manchester na Arsenal mjini, sasa unakwenda kufanyako nini? “ Alisisitiza Mheshimiwa Medard Kalemani.

Awali akiwa katika katika kituo cha redio cha Pangani FM sambamba na ya Mkuu wa wilaya ya Pangani Bi Zainab Abdallah Issa na pamoja na watendaji wengine wa serikali, Mheshimiwa Kalemani amezungumzia kuhusu tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara huku akitaja sababu kubwa kuwa ni miundombinu chakavu, ambapo amesema wataanza kufanya upembuzi na kujenga substation mpya ya kufua umeme katika wilaya ya Pangani ili kuondoa tatizo hilo.



“Kama umeme unakatika ni kwa sababu ya miundombinu na kwa bahati mbaya kuanza Majani Mapana hadi Pangani kuna miti mingi kwa hiyo ikitokea upepo popote pale mti ukagusa nyaya lazima utayumba na kukatika sasa tunachokifanya ni kufanya survey, na tunataka kujenga substation mpya huku Pangani ambayo itakuwa inafua umeme huku huku ili kupunguza umbali mrefu hiyo ndiyo itakuwa ni jitihada kubwa tutakuwa na suluhisho la kudumu vinginevyo kutokana na mabadiliko haya ya hali ya hewa yataendelea kutusumbua lakini mkakati wa kuhakikisha kwamba umeme unakuwa imara katika wilaya ya Pangani ni jambo ambalo tumeanza kulifanyia kazi.” Alisema Mheshimiwa Medard Kalemani.

Wakati wote wa ziara yake wilayani Pangani Mheshimiwa Waziri wa Nishati Medard Kalemani aliambatana na Mkuu wa wilaya hiyo Bi Zainab Abdallah Issa, aliyekuwa Mkurugeniz wa halmashauri ya Pangani aliyesimamishwa kazi hivi karibuni Bwana Sabas Damian Chambasi, pamoja na viongozi wengine wa serikali na chama kutokea wilayani Pangani.

 (Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mivumoni wakifatilia kwa makini wakati Mheshimiwa Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani alipokuwa akizungumza nao)


Ziara ya Mheshimiwa waziri huyo wa Nishati ambayo ilianzia katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Pangani ilikuwa na lengo la kukagua utekelezaji wa mradi wa REA awamu ya pili na tatu ikiwa ni pamoja na kujua changamoto za nishati katika mkoa wa Tanga kwa ujumla.


No comments

Powered by Blogger.