AWESSO AMSHUKIA MWEKEZAJI WA AMBONI PLANTATION KWA KUTOTII MAAGIZO YA SERIKALI


Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mheshimiwa JUMAA AWESSO ameahidi kumchukulia hatua Mwekezaji wa shamba la Mkonge la Amboni Plantation Bwana Hugo Johnson kwa kutotii maagizo ya serikali.


Hayo yamejiri  katika ziara ya siku mbili ya Naibu Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Pangani wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mwera na kusema kuwa mwekezaji huyo ameshindwa kutekeleza agizo lililotolewa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mheshimiwa SULEIMANI JAFFO alilolitoa mwaka jana lililomtaka kumalizia ujenzi wa chumba cha upasuaji kwa wakina mama katika kituo cha afya cha Mwera.

‘’Kuhusu ujenzi huu wa kituo cha afya pamoja na nguvu za wananchi lakini Mheshimiwa Suleimani Jaffo ameagiza muwekezaji wa eneo hili amalizie ujenzi huu, Mheshimiwa mkuu wa Wilaya mpaka sasa hivi mwekezaji yule amekaidi, amekataa, na ameona kwamba hakuna mtu yeyote atakayefanya jambo lolote hiyo ni aibu kubwa sana hususani kwa wilaya yetu ya Pangani, zipo faida ambazo wananchi wanatakiwa wanufaike nazo kutokana na mwekezaji kama vile Afya , Elimu, Maji na kama kuna Miundombinu mibovu ya Barabara basi aborshe ili wananchi waweze kunufaika’’ Asema Mheshimiwa Awesso. 

Ameongeza kwa kuwataka wawekezaji kutatua kero za wananchi wa eneo husika na sio kujinufaisha wenyewe kutokana na uwekezaji.

“Laiti kama wawekezaji wetu wa wilaya ya Pangani kama wanatusaidia hata kisima kimoja kimoja basi wilaya yetu isingekuwa na shida ya maji, hivi kweli anashindwa kutupa sisi mchanga, anashindwa  kuchangia kitu cha maendeleo ambacho hata wafanyakazi wake katika zao la Mkonge watapata huduma? Mheshimiwa mkuu wa wilaya mnyonge mnyongeni haki yake mpeni kwa sisi tufikie hatua ya kuwasaidia wananchi wetu’’Alisema Awesso.

Naibu Waziri huyo wa Maji na Umwagiliaji alifanya ziara ya siku mbili katika jimbo lake la Pangani kwa ajili ya kukagua miradi mbalimbali ya kimaendeleo ili kujipanga kuelekea Bungeni mnamo mwezi ujao.

No comments

Powered by Blogger.