MKANDARASI MSAIDIZI MBARONI KWA KUSUA SUA KWA MRADI WA MAJI PANGANI


Mkandarasi msaidizi wa kampuni ya KHARTON TRADERS LTD Bwana DIKANZA AMIRI MWAYA amekamatwa na kuwekwa ndani na jeshi la polisi wilayani Pangani kutokana na agizo lililotolewa na Naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji nchini Mheshimiwa Jumaa Hamidu Awesso baada ya kutoridhishwa na ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Mtango wilayani Pangani.

Hayo yamejiri wakati wa ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya Maendeleo katika wilaya hiyo ambapo Naibu Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Pangani alipata nafasi ya kutembelea ujenzi huo katika kijiji cha Mtango, Kata ya Mikinguni ili kuona maendeleo ya mradi lakini alishangazwa kuona ukisuasua ambapo aliagiza kusimamishwa kwa ujenzi katika eneo hilo.



Akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Pangani Mheshimiwa Zainab Abdallah Issa, Mkurugenzi wa Halashauri ya Wilaya ya Pangani Bwana Sabas Damian Chambasi na viongozi wengine kutoka halmashauri hiyo, Mheshimiwa Awesso alimweleza mkandarasi msaidizi wa kampuni ya KHARTON TRADERS LTD Bwana Dikanza Amiri Mwaya ya kuwa;

“Hakuna kitu ninachokifuatilia kama huu mradi, nataka uelewe tu na nikueleze kwamza huu mradi ulikuwa unasua sua na hatutasita kuwanyang’anya kama hamko tayari na hamtafanya kazi yenu vizuri kwa sababu sisi kama wizara hatukuwa kikwazo katika kuwalipa pesa zenu, Mkurugenzi nikuambie tu zipo taarifa katika huu mradi kuna baadhi ya vifaa vinauzwa kama ulikuwa hujui, msije mkauza vifaa na mradi ukatoka wa ajabu ajabu hatuta kubali kubambikiwa, na kama mtafanya kazi kiujanja ujanja hamtalipwa’’ Alisema Mheshimiwa Awesso 



Katika hatua nyingine suala la kutokuwepo kwa mkandarasi mkuu wa ujenzi wa mradi huo ambaye alimtuma mwakilishi wake na hivyo kuonekana kutoa ya kubabaisha, lilionekana kumkera Mheshimiwa Awesso na kuagiza mkandarasi mkuu Bwana Karim Mohamed Jiwa kumfuata mkoani DODOMA kwa ajili ya mazungumzo zaidi, lakini badae akiwa kwenye mahojiano na kituo cha redio Pangani FM, alibadili uamuzi huo na kumtaka mkandarasi huyo kufika kwa Mkuu wa Wilaya Zainab Abdallah Issa na ndipo aende Dodoma.

Akizugnumza kwenye mahojiano maalumu kwenye kituo cha redio Pangani Fm, Mheshimiwa Jumaa Awesso alimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Pangani Bwana Sabasi Damiani Chambasi kuwa makini na kitengo cha manunuzi kwa kuhakikisha anawapa tenda watu sahihi watakaofanya kazi kwa ufanisi.



“Kikubwa Mkurugenzi kuna jambo kubwa sana hapa limejificha, cha kujifunza angalia vizuri kitengo chako cha manunuzi tuwape watu  wenye uwezo, na wanaotoa tenda sio mtu ametoa asilimia fulani ya pesa kwa sababu ni sehemu na yeye anatakiwa apate wananchi wa Mtango wanapata tabu, mimi nataka niwahakikishie kama huu mradi hautaeleweka, hakuna mtu atakayelipwa fedha hakuna atakayepata fedha, kwa nini hayupo eneo la kazi mpaka muda huu na kwa nini katuma mwakilishi si kwa sababu kajua mradi hauna kiwango na una kasoro, Mkurugenzi usilale fedha nyingi sana zimetumwa kwa ajili ya mradi huu kama hauta fanya vizuri msimamo wangu upo pale pale hakuna mtu atalipwa fedha, haiwezekani kutekeleza mradi kiujanja ujanja.’’ Amemalizia Mheshimiwa Awesso

Takribani shilingi milioni mia tano (500) zilitengwa kwa ajili ya Ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Mtango, ambapo mpaka sasa Mkandarasi aliyetajwa kwa jina la Karim Mohamed Jiwa kupitia kampuni ya Kharton Traders, ambayo ina usajili wa bodi ya wakandarasi nchini (CRB) kwa namba B6/0591/11/2011, huku ikipewa daraja la sita (6) ameshalipwa shilingi milioni sabini na mbili (72), lakini mpaka sasa mradi bado una suasua.





No comments

Powered by Blogger.