KIJANA PANGANI AENDA JELA MIEZI TISA KWA WIZI WA PESA


Mahakama ya mwanzo ya Mwera wilayani Pangani imemuhukumu Bwana JUMA MIRAJI mwenye umri wa miaka 30 mkazi wa kijiji cha Stahabu kifungo cha miezi tisa jela baada ya kupatikana na hatia wizi wa pesa.

Katika hati ya mashtaka iliyowasilishwa na polisi Mahakamani hapo ilidaiwa kuwa manamo tarehe 15/2/2018 majira ya saa kumi alfajiri mtuhumiwa huyo aliiba jumla ya shilingi LAKI TISA NA ELFU NNE mali ya Bi MWAJUMA HATIBU, ambapo baada ya kusomwa kwa kesi hiyo na kusikilizwa kwa ushahidi wa pande zote mbili za Mahakama hiyo ilimkuta mtuhumiwa huyo na hatia hivyo kuhukumiwa kifungo cha miezi tisa jela na akitoka amlipe mlalamikaji fidia ya kiasi hicho cha pesa.

Wakati huo huo Mahakama hiyo pia ilitoa hukumu kwa Bwana SHEKHE OMARI mkazi wa kijiji cha Mzambarauni wilayani Pangani mwenye umri wa miaka 55, kumlipa faini ya shilingi laki 5 au kwenda jela miezi 12 baada ya mifugo yake kula mazao ya Bwana JOSEPH PAUL ambaye ni Mkuu wa Takukuru wilaya ya Pangani.

Katika hati ya mashtaka iliyowasilishwa mahakamani hapo ilidaiwa kuwa mnamo tarehe 18/2/2018 na tarehe 20/2/2018 mifugo ya Bwana SHEKHE OMARI iliingia katika shamba la Bwana JOSEPH PAUL na kula Migomba na Viazi na kusababisha hasara ya jumla ya shilingi Milioni Moja Laki Moja na Elfu Sabini.

Mtuhumiwa huyo alilipa faini hiyo ya shilingi laki 5, pamoja na kumlipa mlalamikaji kiasi hicho cha shilingi million moja laki moja na elfu sabini kama fidia na hivyo kuachiwa huru.

Hukumu zote hizo zimetolewa na hakimu mfawidhi wa mahakama ya mwanzo ya Mwera Bwana ANTONI HAMZA.

No comments

Powered by Blogger.