DC PANGANI 'KULA SAHANI MOJA' NA WAWEKEZAJI WASIO NA TIJA


Mkuu wa Wilaya ya Pangani Bi Zainab Abdallah Issa amesema kuwa umefika wakati sasa wawekezaji wote wasiona tija Wilayani Pangani kutovumiliwa kufuatia uwekezaji wao kutokuwa na manufaa ya kuleta Maendeleo wilayani humo.
 
Akizungumza na Pangani FM hivi karibuni Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa, umefika wakati wa kuwaondoa wawekezaji wote wanaoshindwa kuchangia katika miradi ya kimaendeleo, ilhali wao wananufaika kwa kiasi kubwa na rasilimali zilizotunzwa vizuri na wanapangani wenyewe.

Nachukuwa nafasi hii pia nimuombe Mkurugenzi na wataalamu wake, ifike mahali msikae kimywa, haya mambo mengine hayavumiliki hii ni wilaya yetu, kuna baadhi ya wawekezaji wilayani kwetu hawana tija, hivyo wanapaswa kufahamu kwamba sisi ndio serikali na sisi ndio dola hapa wilayani hatumuogopi mtu, kuna watu wanavimba huko mitaani wakiamini wao wana pesa na wana miradi mikubwa ya uwekezaji hapa wilayani Pangani lakini kwetu hawana tija yeyote” Amesema Bi Zainabu.

Pamoja na hayo Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa mpango alionao ni kuhakikisha anakutana na wawekezaji wote waliopo wilayani humo kwenye kikao maalum, huku akikemea kitendo cha wawekezaji pindi wanapoitwa kutuma wawakilishi wao.

“Kwa hiyo na mimi natuma salamu zangu kwa wawekezaji wa hapa wilayani Pangani, nitakuwa na kikao na wawekezaji wote na kuna desturi kuna mtu akisikia kuna kikao anatuma muwakilishi mtu ana tuma hadi dereva wake aje kuwakilisha kwenye kikao, hebu fikiria dereva kweli? Sasa ifike mahala tufunge ofisi zao na waje kwenye kikao ili wajuwe serikali ipo, tunaenda nao kiubinadamu na kistaarabu lakini tunashindwa kuheshimiana basi tuchukuwe hatua kali, leo tunashindwa kujenga hata kituo cha Polisi tunaomba msaada nje wakati wapo wawekezaji wa hapa ndani na wanatumia rasilimali za wilaya hii lakini hawajaona umuhimu wa kusaidia wananchi’’ Alimalizia kwa msisitizo Mkuu wa Wilaya.

No comments

Powered by Blogger.