"WANAWAKE PANGANI HAKUNA KUKATA TAMAA"- AFISA UTUMISHI
Wanawake wilayani Pangani wametakiwa kutokata tamaa
katika utafutaji wa kipato ili kujiletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Hayo yamezungumzwa na Afisa Utumishi wa Halmashauri
ya wilaya ya Pangani Bi Mwanaidi Nondo wakati akizungumza na Pangani Fm ofisini
kwake na kuongeza kuwa mwanamke akikata tamaa hawezi kufika mbali hivyo
amewasihi kujituma kwa bidii ili kuiletea jamii mabadiliko.
‘’Mimi
nawashauri wakina mama wenzangu tusikate tamaa kwa sababu unapojikatia tamaa
mwenyewe huwezi kufika mbali, kweli tuna changamoto nyingi tunazozipata kwenye
utendaji wa kazi mambo ya biashara na kifamilia yaani kikubwa ni kutokukata tamaa,
tujipe moyo, kwani nina imani kuwa wanawake tunaweza kama tukijiamini basi
tutafika mbali.’’ amesema Bi Mwanaidi.
Amesema Halmashauri ya Pangani imejipanga vizuri
kuadhimisha siku ya wanawake duniani ambapo kiwilaya itakayofanyika kijiji cha
BOZA kata ya KIMANG’A na kuwasihi wanawake kujitokeza kwa wingi katika sherehe
hizo.
‘’Kama halmashauri tumejipanga vizuri kuadhimisha siku ya wanawake
duniani inayotarajiwa kufanyika tarehe 8/3/2019 na tumejipanga vizuri na
tumetoa ushirikiano mkubwa sana ili tufikie malengo ya siku hii, hivyo nawashauri
kina mama tujitokeze kwa wingi ili tubadilishane uzoefu’’ amesema Bi Mwanaidi.
Kauli mbiu ya mwaka huu 2019 ya maadhimisho ya siku
ya mwanamke duniani inasema kuwa “badili fikra kufikia usawa wa kijinsi kwa
maendeleo endelevu”.
No comments