WANANCHI PANGANI WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA MAHAKAMA ILI KUPATA HAKI ZAO
Wananchi wilayani Pangani na nje ya Wilaya hiyo
wametakiwa kushirikiana na Mahakama ili kurahisisha kumaliza mashauri kwa
haraka kwa mujibu wa sheria ili haki iweze kupatikana kwa wakati.
Akizungumza wakati wa kipindi cha Asubuhi ya leo
kinachorushwa na Pangani FM Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mwera pamoja na eneo la Mkalamo Bwana Antony Clement Hamza amesema kuwa wananchi wanatakiwa kutimiza
yale wanayoamriwa kwa kutoa ushirikiano ili kuirahisishia Mahakama utekelezaji
wake kwani wapo tayari kuwasikiliza.
‘Tupo tayari kuwasikiliza watimize yale ambayo
wanaamriwa kwa ajili ya kufikia zile haki zao ambazo wanataka kuzipata na hiyo
itasaidia ule utaratibu wetu wa kusikiliza maashauri kwa wakati na kutoa
maamuzi kwa haraka, wasipotoa ushirikiano kwa kutimiza yalioamriwa na maelekezo
yaliyoamriwa basi yataweka mkwamo kwa kufikia malengo kwetu sisi kwa kumaliza
mashauri haraka na wao kupata haki kwa wakati” Amesema Bwana Hamza.
Kwa upande wake Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo
mjini Pangani Bwana PAUL MAGESA
amewataka wananchi kufika katika Mahakama ili kujifunza sheria
mbalimbali na kufahamu sehemu ya kuweza kupata haki zao za kimsingi.
“Kwanza waione Mahakama ni chombo chao kwa hiyo
wafike Mahakamani si lazima wasubiri siku za elimu ya sheria, vile vile wapende
kujifahamisha zaidi taratibu, zipo taasisi mbalimbali zinazotoa elimu ya msaada
wa sheria lakini zaidi kabisa ni kuwa na uelewa kwamba nikiwa na haki yangu
naipata wapi kwa maana ni jambo la kwenda Mahakamani usipoteze muda kwa kupita
katika ofisi nyingine ambazo hazitakupa majibu kwenye jambo lako nenda kwenye
chombo husika uweze kupata haki yako” Amesema Bwana Magesa
Katika kuelekea juma la sheria nchini Tanzania ambalo lilianza Januari 27 mwaka huu, Hakimu Antony Hamza amesema tayari wameanza kutoa elimu
kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ikiwemo sokoni mjini Pangani pamoja na Mahakamani kuhusu sheria mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wa sheria ikiwemo
jeshi la Polisi, TAKUKURU na wasaidiazi wa kisheria PACOPA.
Hayo yamekuja
wakati nchi ya Tanzania ikielekea kuadhimisha siku ya sheria nchini itakayofanyika tarehe 1/2/2018.
No comments