PANGANI YAZIDI KUPIGA KASI KIMAENDELEO, SASA KUJENGWA KITUO KIPYA CHA KISASA CHA POLISI



 (Mkuu wa wilaya ya Pangani Bi Zainab Abdallah Issa akizungumza wakati wa mkutano na wadau wa maendeleo Pangani kuhusu ujenzi wa kituo kipya cha polisi)
Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Pangani Bi ZAINABU ABDALLA ISSA amekutana na wadau muhimu wa Maendeleo wilayani humo kwa lengo la kujadili hali ya kituo cha Polisi cha Pangani pamoja na kuweka mikakati ya ujenzi wa kituo kipya cha kisasa ili kuboresha huduma za kipolisi.

Akizungumza wakati wa Kikao hicho Bi ZAINABU amewaomba wadau hao kusaidia ujenzi wa kituo hicho kipya cha polisi ambacho kitakuwa cha kisasa ili kuboresha huduma za kipolisi zitakachowezesha kupatikana kwa askari wengi na kutoa huduma bora sawa sawa na hadhi ya kiwilaya.

“Mpaka sasa hivi tayari tumeshafanikiwa kukusanya mifuko 450 ya simenti, lakini pia tumefanikiwa kukusanya nondo 150 na tunamshukuru sana Mheshimiwa mbunge Jumaa Awesso kwa kuongezea kisima cha maji, kwa hiyo tunaomba sasa wadau mtusaidie." Alisema Mkuu huyo wa Wilaya na kuongeza kuwa..

"Tumejipanga kama serikali tukawe na kituo cha hadhi daraja la kwanza kabisa ya kituo cha polisi na ikibidi kikawe mfano katika mkoa wa Tanga, lakini leo tukiwa na kituo kikubwa cha polisi maana yake hata watumishi nao wataongezeka na huduma kwetu sisi wananchi zitakuja kwa haraka kwa kuwa hata bajeti inaongezeka”. Alisema Bi Zainab.

 (Naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Pangani Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso akizungumza wakati wa mkutano huo)


Kwa upande wake Naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Pangani Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso ameahidi mifuko mia mbili ya saruji  pamoja na kuahidi kuchimba kisima kikubwa cha maji ili  kuhakikisha katika kituo hicho kinakuwa na huduma bora.

“Katika hili mimi kama Mbunge wa Pangani nimeahidi kuwa nitatoa mifuko mia mbili ya sementi katika kuhakikisha kwamba tunaanzisha hili jambo, lakini la pili maeneo ambayo kile kituo cha Polisi kitakapojengwa lazima kuwe na mazingira ya kupatikana vitu muhimu, mimi kwa nafasi niliyonayo ya unUnaibu Waziri wa Maji Ocd nitakuchimbia kisima pale kikubwa tu katika kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa ukaribu” Alisema Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso.



(Katibu mteule wa kamati ya ujenzi wa kituo kipya cha Polisi Pangani Ndugu Novatus Urassa ambaye pia ni Mkurugenzi wa shirika la Uzikwasa wakati wa mkutano huo)

Mbali na baadhi ya wadau kutoa ahadi mbalimbali katika ujenzi huo, mkutano huo pia ulifanikiwa kuunda kamati ndogo kwa ajili ya kufuatilia ahadi zilizotolea ambapo baada ya uteuzi, Katibu mteule wa kamati hiyo Ndugu Novatus Urassa ambaye pia ni Mkurugenzi wa shirika la Uzikwasa amesema wanatarajia kukutana wajumbe wote wa kamati hiyo kwa ajili ya kuweka mikakati ya kusimamia ujenzi huo.

“Na kamati hiyo ina wajumbe wanne ambao wamechaguliwa, Mwenyekiti ni Mohamedi Rishedi aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Pangani, Msaidizi ni Bwana Husein Magati, Katibu nimechaguliwa mimi Mr URASA kutoka Shirika la UZIKWASA na mweka hazina ni Mr ABELI Meneja wa Benki ya NMB Pangani na msaidizi wake Bwana Kenethy Patrick kutika jeshi la polisi Pangani.” Amesema Bwana Urassa na kuongeza…

“Tutakutana kuweka mikakati kwamba ni kwa namna gani sasa tunaweza tukaanza kazi  na baadae tutakutana na mkuu wa wilaya aweze kutupa hadidu rejea kwamba namna gani tuanze kazi hiyo, twende namna gani tuweze kufanikisha jambo hilo muhimu kwa wilaya ya Pangani”. Alisema Bwana Urassa.

 (Kamanda wa polisi wilayani Pangani Bi Christina Musyani akisikliza kwa makini wakati wa kikao hicho)


Inakadiriwa kuwa ni miaka 60 imepita tangu kujengwa kituo cha polisi cha wilaya ya Pangani ambapo inaelezwa kuwa wakati kinajengwa miaka hiyo hakikujengwa kwa ajili ya matumizi ya  kituo cha polisi hivyo kusababisha kutopatikana kwa huduma bora za kipolisi.



No comments

Powered by Blogger.