TAMAPENDO- Tamthilia Mpya Ya UZIKWASA Wilayani Pangani




Kwa mara nyingine tena shirika la UZIKWASA lililopo wilayani Pangani limekuja na mambo mapya. Safari hii ni tamthilia ya mchezo wa redio unaofahamika kama Tamapendo.
Lengo la tamthilia hii ni  kuonesha changamoto za vijana wawili kujiendeleza katika maisha yao katika jamii ambapo kanuni za unyanyasaji wa kijinsia za kijamii bado zinashinda.

Tamapendo inakuwa tamthilia ya pili ya redio kutengenezwa na shirika la UZIKWASA baada ya mchezo wa redio wa Penye Nia…..uliopatwa kusikilizwa na jamii nzima ya Pangani kupitia kituo cha redio cha Pangani FM, ambacho pia kinamilikiwa na shirika la UZIKWASA wilayani Pangani.

Shirika hili pia limekuwa na utaratibu kutengeneza filamu mbali mbali hasa kuhusu masuala ya haki na ukatili wa kijinsia.  Kutokana na utafiti wa ndani kabisa filamu za UZIKWASA zinasimulia story halisi za jamii ya Pangani na zilifanikiwa kugusa watamazaji kwa sababu filamu hizi ni kama kioo cha changamoto zao. 

Filamu hizo ni  Fimbo ya Baba ambayo ilitengenezwa mwaka 2006, Chukua Pipi iliyotoka 2012 na  filamu maarufu ya  AISHA ya mwaka 2015.  AISHA ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa, siyo Pangani tu, lakini Tanzania nzima na nchi nyingi za kimataifa. Imepata tuzo mbalimbali kimataifa kutoka tamasha za filamu maarufu USA na Africa. 

Pamoja na hayo yote, sasa shirika la UZIKWASA limekuja tena na tamthilia ya redio inayoitwa Tamapendo. Kama kawaidi ya filamu na tamthilia ya redio za UZIKWASA karibu waigizaji wote hutokea Pangani. 

Na ndivyo ilivyotokea kwa Tamapendo ambayo imeongozwa kwa ushirikiano na wagurugenzi wa mchezo Chande Omar na Irene Sanga. Story ya tamthilia hii inatokana na tafiti iliofanyika na UZIKWASA pamoja na mchango wa wanajamii wa Pangani.  
Tamthilia imetengenezwa na kuhaririwa kwenye studio ya redio Pangani FM –Sauti ya Jamii.

Tamapendo ni kuhusu nini?

Ni story ya vijana wawili Fatuma na Chaballa wanaokutana na dhuruba kubwa ya maisha.  Wanajiona kuelemewa na mambo mazito kuhusiana na ukatili mbalimbali na dharau kuhusiana na haki za wanawake na wasichana.

Wakati wakijinusuru kutetea upendo wao wa dhati na kufuatilia ndoto zao katika maisha, wanajikuta kunaswa na mtego wa tamaa unaotawala kijijini kwao.  

Ni matumaini ya UZIKWASA kuwa Tamapendo ambayo tayari imeshazinduliwa, itazunguka nchi nzima ili kuwafikia wasikilizaji wengi na kuibua mijadala.



No comments

Powered by Blogger.