FAHAMU YALIYOJIRI PANGANI WAKATI WA ZIARA YA MHESHIMIWA MWIGULU NCHEMBA
Serikali
kupitia wizara ya mambo ya ndani ya nchi imejipanga kuhakikisha idara zote
zilizopo chini ya wizara yake, zinazingatia maadili kwenye nafasi zao katika
utekelezaji wa shughuli zake ili serikali iweze kufikia malengo yake.
Akizungumza
katika studio za Pangani fm waziri mwenye dhamana kupitia wizara ya mambo ya
ndani ya nchi Mheshimiwa Dk Mwigulu Lameck Nchemba, amesema kuwa mara zote
serikali imejidhatiti katika kuhakikisha wizara zote zinawaletea manufaa
wananchi wake, huku akipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kutowafumbia macho
watu kwenye jamii na hata watendaji wa serikali wanaobainika kwenda kinyume na
matakwa ya serikali.
“Tumejidhatiti,
utaweza kuona kwamba kwenye kila jambo ambalo serikali imeweka agenda yake
maalum, pakitokea mtendaji hata raia akaenda kinyume na hayo amekuwa akifika
katika mkono wa sheria, utaona kwenye vita ya madawa ya kulevya tumeweza
kuchukua hatua na hii ni kwa sekta zote” Amesema Dk Nchemba na kuongeza kuwa.
“Hata
wale ambao walikuwa kwenye vyombo vya haki na wakashindwa kutoa haki kwa
kutokwenda na kasi ya vita ya madawa ya kulevya hata wenyewe walichukuliwa
hatua, hata wachukuaji wa hatua ambao walistahili kuchukua hatua, pale
palipoonekana hawakuchukua hatua, hatua zilichukuliwa dhidi yao. Kwa maana hiyo
hakuna mchezo unaposikia hapa kazi ni kazi tu kweli kweli” Amesema Waziri wa
mambo ya ndani Dk Nchemba.
Dk Nchemba ameongeza kuwa serikali ya awamu ya tano imetenda mengi mema katika mkoa wa Tanga kwa kuhakikisha inawapa viongozi vijana wenye kasi katika utendaji wao wa kazi kuanzia mkuu wa mkoa, wilaya na hata mbunge kwenye jimbo la pangani, na kuongeza kuwa ili halmashauri hiyo ipige hatua ni muhimu pia kuwatumia wafungwa katika shughuli za ujenzi wa taifa..
“Sehemu ya
Magereza, wale waliopo kule tumesema tunawapeleka kwaajili ya urekebishwaji na
kuna watu wako na vipaji vyao, ni faida na ni kitu chema kwa serikali
kuhakikisha kwamba hawa watu hawatumii tu kodi za watanzania waliowema
kuwalisha wao waliokuwa wamevunja sheria, kwa maana hiyo hili ni sharti kwamba
lazima watumike kwenye shughuli za uzalishaji na si tu uzalishaji wa chakula,
kuwatumia pia katika shughuli nyingine
za ujenzi wa taifa” Amesema Dk Mwigulu waziri wa mambo ya ndani.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso
ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Pangani aliyeambatana na waziri Nchemba
amesema kuwa, mara zote ataisemea Pangani hivyo katika suala la makazi bora kwa
askari polisi jimboni mwake atachangia mifuko mia mbili ya Saruji.
Sisi
kauli mbiu yetu, anayelala na mgonjwa ndie anayejua mihemo yake kwa hiyo aone
hali halisi ya wafanyakazi wa jeshi la polisi. Unaweza ukawa baba wa watoto
sita lakini siku ukatoka kazini ukaja na shati ukampa Saidi sio kama Abdalla na
wengine sio watoto wako hapana. Tunajua majeshi yapo mengi sana lakini wa
wilaya ya Pangani wanahitaji kusaidiwa, hata wagonjwa kuna wengine wapo hoi
wanatakiwa wapelekwe sehemu ya dharura ICU”. Amesema Mh Aweso na kuongeza kuwa.
“Hata
sisi Pangani tupo ICU tunakuomba angalia namna ya kutusaidia kituo hiki cha
polisi na mimi kama mbunge kwenye mfuko wangu wa jimbo nitawapa mifuko 200 ya
sementi kuchangia jitihada hizi katika kuhakikisha tunaboresha makazi ya
askari”. Amesema Mh Jumaa Aweso Mbunge wa Jimbo la Pangani.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Pangani Bi Zainab Abdallah Issa ambaye pia ni mwenyekiti wa
kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani humo amesema kuwa, ujio wa Mheshimiwa
Nchemba umekuja na mambo mengi hasa kuimarisha utendaji wa idara chini ya
wizara yake, kwa kuhakikisha pia kunafanyika doria za mara kwa mara.
“Kwa
kweli ni faraja kubwa kwa wanapangani, kwa sababu katika wizara ya mambo ya
ndani kuna taasisi nyingi sana ambazo moja kwa moja zinaenda kuwagusa wananchi,
pia nimshukuru kwa kutuletea gari kwa sababu jeshi letu la polisi tulikuwa na
changamoto ya magari kwa hiyo kitendo cha wizara kutuletea gari maana yake
kimeongeza ufanisi, usimamizi utaboreshwa na huduma zitaenda haraka kwa
wananchi”. Amesema Mkuu huyo Bi Zainab.
Waziri
wa mambo ya ndani ya nchi Mhe Mwigulu Lameck Nchemba amekuwa katika ziara fupi
ya kikazi Wilayani Pangani kuanzia tarehe 4 hadi 5 February 2018, ambapo pamoja
na shughuli nyingine pia amehudhuria uzinduzi wa kampeni za chama cha mapinduzi
CCM huko katika kata ya Madanga.
No comments