PANGANI HAIKAMATIKI, SERIKALI KUJENGA BARABARA PAMOJA NA DARAJA LA KISASA.



Katika kuboresha na kuimarisha miundombinu nchini Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mheshimiwa Elias Kwandikwa amewahakikishia wananchi wa wilaya ya Pangani Mkoani Tanga  kuanza rasmi kwa ujenzi wa barabara kutoka Tanga-Pangani-Sadani hadi Bagamoyo, ikiwa ni pamoja na kuelekea uchumi wa kati  kama lilivyo tamko la serikali ya awamu ya tano.

Mheshimiwa Kwandikwa ameyasema hayo wakati alipokuwa kwenye ziara yake Wilayani humo kwaajili ya kuangalia miundombinu ya barabara hiyo na kusema kuwa tayari serikali imetenga fedha kwaajili ya ujenzi utakaoanza mwaka huu, ambapo pia itaambatana na ujenzi wa daraja kubwa na la kisasa pamoja na kuimarisha kivuko kilichopo katika Mto Pangani.

“Niwahikikishie tu wanapangani na watu wa Tanga na watanzania kwa ujumla, hii barabara ambayo leo tumeipita tumeshaanza kuijenga kwa maana imeshasanifiwa, na tumebakia sasa kuipatia fedha iweze kuanza kujengwa, muda si mrefu mtaona harakati za ujenzi zinaanza” Amesema Mheshimiwa Kwandikwa na kuongeza kuwa


“Nataka niwatoe wasiwasi barabara tunajenga, lakini nilikuwa naangalia kivuko hiki, kitakuwa muhimu kwasababu kitatusaidia wakati wa ujenzi wa barabara tutahitaji siment ivuke huku kwasababu barabara hii haitaishia hapa itakwenda mpaka itoke kule Bagamoyo nyie mnajua, itapita kandokando ya Saadani ili watalii wengi waende, wakipita watalii hapa mwenye biashara yake atafanya na nyie vijana mtapata ajira”. Amesema Mheshimiwa Kwandikwa.







Hata hivyo Mheshimiwa Kwandikwa amezungumzia umuhimu wa kuboreshwa kwa barabara, daraja na kivuko hicho, na kusema kuwa ujenzi wa barabara hiyo iliyokuwa ikisemewa kwa muda mrefu, kukamilika kwake kutachangia kuinua wafanyabiashara wadogo wadogo kiuchumi na hatimaye kuongeza pato la taifa. 

“Tutakuwa na ile barabara lakini kutakuwa na mradi mwingine wa ujenzi wa lile daraja ni kubwa na la kisasa lina mita mia tano karibu na hamsini kati ya madaraja makubwa ya Tanzania itakuwa kati yake ambalo pia litaupamba mji wa Pangani, ni daraja ambalo litakuwa la kisasa ambalo litakuwa linaweza kupita meli chini na magari yanapita juu, hii itaturahisishia sana kwa usafiri mtu akitaka kwenda Dar es Salaam hatapita Tanga tena bali atapita Pangani atavuka aende zake” Amesema Kwandikwa na kuongeza kuwa…..

“Hili liko kwenye mpango wa serikali na suala la fedha nafikiri liko mbioni. Fedha zije haraka twende kujenga, sisi tunataka ule muunganiko na nyororo wa huduma, kwahiyo tutapandisha uchumi wa Pangani na kwa upande wa serikali tumejipanga, na sisi tunajua kabisa kwamba miundombinu inachangia asilimia 80 ya ukuaji wa  uchumi”. Amesema Mheshimiwa Kwandikwa.



Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Elias Kwandikwa amewataka wananchi wote kushirikiana vyema na viongozi wao ili kuweza kukamilisha ujenzi wa barabara, Daraja na kivuko hicho, akisema serikali imeamua kurahisisha huduma mbalimbali kwa wananchi wake ambazo ni pamoja na usafiri.

No comments

Powered by Blogger.