KAMATI YA SHULE YA MSINGI KIJIJI CHA SANGE (W) PANGANI YAAHIDI MSHIKAMANO
(Bwana Donald Katanji akifanyiwa mahojiano na mwandishi wa Pangani Fm Mohammed Hammie)
Kamati ya Shule ya Msingi kijiji cha
Sange Wilayani Pangani kwa kushirikiana na wazazi imeahidi kuweka mshikamano
katika kupambana na changamoto ya suala la ukatili kwa watoto ambalo
limejitokeza wakati wa mafunzo ya Minna dada yaliyodumu kwa muda wa siku tatu
katika kijijini hapo.
Akizungumza wakati wa hitimisho la
mafunzo hayo mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambae pia ni katibu wa kitongoji
cha Sange Kuu Bwana DOLDAN KATANJI, amesema kuwa suala la kutokomeza ukatili
kwa watoto linapaswa kuwa na mshikamano ili kumnusuru mtoto katika madhila
hayo.
“Ni kwamba tushirikiane pamoja kuanzia
wazazi, kamati, sisi viongozi wa vitongoji na vijiji, tushikamane na wadau
mbalimbali ili tuweze kumuondoa mtoto huyu katika madjila ya kufanyiwa vitendo
vya ukatili ili sasa ajitambue kwamba yeye ni nani” Amesema Bwana Katanji.
(Mjumbe wa
kamati ya shule ya msingi ya kijiji cha Sange Bi NINJAMA BAKARI akilia baada ya kushindwa kuvumilia taarifa ya utafiti wa ukatili kwa watoto iliyotolewa wakati wa mafunzo hayo)
Kwa upande wake mjumbe mwengine wa
kamati hiyo Bi NINJAMA BAKARI
ameonesha kusikitishwa na taarifa ya ukatili kwa watoto iliyotokana na
utafiti uliofanywa na kundi la Banja Basi
baada ya kuzungumza na watoto wa eneo hilo kupitia mfumo salama wa
kuripoti matukio ya kikatili, ambapo aliitaka kamati hiyo kutambua na kutekeleza
majukumu yao.
“Toka semina yetu ianze mpaka hivi leo
nimejifunza mengi, na nikianza kuyasema yanayoniuma ndani ya nafsi sitaweza
kuyamaliza, kubwa zaidi ambalo limeniumiza ni hii orodha ambayo ameitoa
mkufunzi! Watoto wengi wameathirika na mimi ni mzazi, pamoja na kwamba wa
kwangu hajatajwa siwezi sema kama yuko salama! Roho inaniuma, inaniuma vibaya,
kamati hii itambue majukumu yake” Amesema Bi Ninjama.
Kwa upande wake Afisa ufuatiliaji na
tathmini pamoja na utafiti kutoka shirika la Uzikwasa Bwana KENNEDY MASHEMA, amewaeleza wajumbe wa
kamati hiyo kuwa tayari shirika hilo lina mfumo salama wa kutolea taarifa
matukio ya ukatili kwa watoto, ambo huwa wanafundishwa namna ya kutoa taarifa hizo kwa walimu na
walezi wawapo shuleni.
“Ni mfano ambao tunautumia katika
kurekodi kumbukumbu za ukatili kwa wototo, na hizi kumbukumbu lazima ziwe zina
mfumo rasmi, ambao kwa wale watoto 14 ambao tumefanya nao majadiliano tukapata
taarifa huwa wanawakilishwa na kila darasa watoto wawili mvulana na msichana” Amesema
Bwana Kennedy Mashema na kuongeza kuwa…
“Kwa hiyo wale watoto wamefundishwa
namna gani ya kugundua masuala mazima ya ukatili, akikuona unamkonyeza anajua
kuwa hii ni ishara ya kwenda kufanyiwa ukatili. Kwa hiyo wamefundishwa namna ya
kuja kuripoti kwa mwalimu mkuu au mwalimu mlezi wa kiume (Patron) au mwalimu wa
kike mlezi (Matron)” Amesema Afisa huyo ufuatiliaji na tathmini pamoja na utafiti
kutoka shirika la Uzikwasa.
Kambi ya mafunzo ya Minna dada
imemalizika rasmi jana kwa tamasha kubwa la sanaa kutoka kundi la BANJA BASI,
huku likipambwa na onesho la vidokezo vifupi vya video yaani video spot pamoja
na sinema.
No comments