JESHI LA POLISI PANGANI LAWASHUKURU WANANCHI WA MADANGA



Jeshi la polisi wilayani Pangani mkoani Tanga limewashukuru wananchi wa kata ya Madanga kwa kushiriki vyema katika uchaguzi mdogo wa Marudio ulifanyika February 17 mwaka huu.

Akizungumza na Pangani fm Kamanda wa polisi wilayani humo Bi Christina Musyani, amesema kuwa shughuli zote za uchaguzi mdogo wa marudio katika kata ya Madanga zimefanyika salama na kwa haki, na kuongeza kuwa kama jeshi Polisi lilihakikisha kila aliyestahili kupiga kura siku hiyo anapiga kwani ni haki yake kikatiba.

’Baada ya uchaguzi napenda kuwashukuru wananchi wa Madanga ambako ndiko kulikuwa zikiendelea shughuli za uchaguzi kwa ajili ya kumpata diwani wa kata hiyo, uchaguzi umefanyika ukiwa salama, umefanyika kwa kila aliyekuwa anatakiwa kupiga kura alipata haki yake ya msingi’’ amesema Musyani.



Aidha Kamanda Musyani amesema kama jeshi la polisi litahakikisha usalama wa Pangani muda wote, hivyo amewataka wananchi kushirikiana na jeshi hilo pamoja na viongozi  wao ili waweze kuleta maendeleo kwenye maeneo yao.

’Nawashukuru sana tuendelee kuwa watu wa amani na kuimarisha amani tuendelee kuwa salama na tunataka Pangani salama na Madanga salama’’ ameongeza Musyani.

Katika uchaguzi huo mdogo wa marudio katika kata ya Madanga Wilayani Pangani, Mgombea udiwani kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM Ndugu Athumani Tunutu Mnguu aliibuka kidedea kwa kupata kura 661, akimpita mpinzani wake Bwana Swahibu.J. Mwanyoka wa Chama cha Wananchi CUF aliyepata kura 602 na Bwana Mohammedi Abdallah wa ACT-Wazalendo aliyepata kura 12.

No comments

Powered by Blogger.