HALMASHAURI YA PANGANI YADHAMIRIA KUMALIZA UJENZI WA KITUO CHA AFYA MWERA KWA WAKATI
Halmashauri ya Wilaya ya Pangani imeanza mchakato
katika Mradi wa kuboresha kituo cha Afya kilichopo eneo la Mwera kwenye utoaji wa huduma, mradi ambao
unatakiwa kukamilika ndani ya siku tisini tangu ulipoingiziwa fedha.
Wakiameambatana kwa Pamoja katika mazungumzo maalum
na kituo cha Pangani Fm, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani
Daktari Juma Mfanga na Msimamizi wa Miradi mbalimbali ya kimaendeleo wilayani
humo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Bwana Sabas Damian
Chambasi, wamesema kuwa kiasi cha fedha Milioni 400 ambacho wamekipokea kutoka
serikali kuu, zinapaswa kutumika ipasavyo kwa ushirikiano wa pamoja, ili
kuhakikisha ndani ya miezi mitatu mradi huo unakamilika kama inavyotakiwa.
Kwa upande wake Bwana Sabas amehimiza ushirikiano wa
pamoja katika hatua za awali mpaka kukamilika kwa mradi, ndio msingi wa
kukamilika kwa wakati.
“Mnamo tarehe Desemba 27, 2017 Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ilituletea fedha kiasi cha shilingi milioni Mia Nne,
hizi fedha zimekuja zikiwa na muongozo lakini huo muongozo unatuhitaji sana
tushirikishe wananchi katika kuhakikisha kwamba hizo fedha zinatumika”. Amesema
Bwana Sabas Chambasi na kuongeza kuwa……
“Tunataka kwenda kuboresha kituo cha afya Mwera
inatakiwa ushirikiano kati ya serikali, wananchi na wadau mbalimbali wa
maendeleo, siku ambazo tumepewa kwa ajili ya kukamilisha mradi kuanza na
kukamilisha mradi ni siku tisini tu maana yake ni nini miezi mitatu tu, ili
kukamilisha mradi huu inatakiwa wote tushirikiane katika kununua, kuhakiki,
tuanze kwa pamoja na tumalize kwa pamoja tukiwa na kasi mpaka tunamaliza”.
Amesema Mkurugenzi huyo
Kwa Upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya
ya Pangani Dokta Juma Mfanga, mbali na kusema mradi huo unakwenda sambamba na
kuongeza wataalam katika kituo hicho, pia amesema ziko fedha nyingine zilizotengwa
kwaajili ya kununulia vifaa tiba.
“Kama kituo kikikamilika kesho tungeendelea kufanya
upasuaji mana sisi katika hospitali ya halmashauri tuko saba pamoja na kwamba ikama ya madaktari inasema hospitali ya
wilaya iwe na madaktari nane wenye digree ya miaka mitano, lakini population ya huku ni ndogo kuliko
wilaya nyingine, ila shuleni wako wawili wanasoma wakirudi wanakuwa tisa. Kwa hiyo kumtoa mtaalam kumpeleka pale sio
tatizo na juzi tumepata wengi tu wa ajira mpya na wengi tumewapeleka pale makusudi
kwa sababu baada ya miezi mitatu kituo kitaanza kufanya kazi”. Amesema Bwana
Mfanga na kuongeza kuwa…..
Daktari Mfanga ameongeza kuwa katika suala la Afya
hakuna siasa wala dini, hivyo uboreshaji wa kituo cha Afya Mwera ni suala
linalopaswa kutekelezwa na watu wote bila kujali itikadi zao, akisema maendeleo
ni suala linaloletwa kwa pamoja na si kwa kujitenga.
“Ni vizuri watu wakaelewa kitu kimoja katika suala
la afya hakuna siasa ukishakuwa unaumwa hautibiwi na hospitali ya chama fulani
au ya dini fulani, sisi kazi yetu ni kusimamia kazi za serikali na tuko hapa
kwa ajili ya serikali, kwa hiyo katika suala la kituo cha afya Mwera linatakiwa
kutekelezwa na watu wa dini zote pia vyama vyote”. Amesema Daktari Juma
Tarehe 27 mwezi wa 12 mwaka jana wa 2017, serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliingizia halmashauri ya wilaya ya Pangani
kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya uboreshaji wahuduma za afya katika
kituo cha Mwera, huku halmashauri hiyo ikipewa siku tisini yaani miezi mitatu
kuhakikisha mradi huo unakamilika kama inavyopaswa.
No comments