VMAC KIJIJI CHA KIMANG'A WAIBUA MAOVU YA UBAKAJI BAADA YA KUTEMBELEWA NA UZIKWASA



Baadhi ya wanawake katika kijiji cha KIMANG’A Wilayani Pangani wameeleza hofu yao katika kutekeleza shughuli mbali mbali za kimaendeleo ikiwemo za mashambani baada ya kuwepo kwa matukio ya ubakaji, ambayo kwa sasa hayajali rika.

Hofu hiyo iliyoelezwa na wanawake hao imetokana na tukio la ubakaji walilolifuatilia punde walipotoka kupatiwa mafunzo ya mguso, lililotaka kumkuta mwanamke mwenye umri unaokadiriwa kuwa wa miaka hamsini hadi sitini, aliyetaka kubakwa na kijana anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya kumi na tisa hadi ishirini na tatu.

Wakieleza kwa hisia, wajumbe wa kamati ya kudhibiti Ukimwi Jinsia na Uongozi VMAC ya kijiji hicho, mara baada ya kukutana na shirika la UZIKWASA katika mafunzo saidizi yanayowalenga viongozi waliopatiwa mafunzo ya mguso, wamesema vitendo hivyo havikubaliki kwani vinaendelea kudhalilisha utu wa mwanamke kila uchwao.


Pamoja na tukio hilo lililoacha wazi vinywa vya walio wengi, wajumbe wa kamati ya VMAC ya kijiji hicho wameshauriana isiwe mwanzo, bali waendelee kuibua matukio mbalimbali, kwa kuhakikisha wanayafuatilia kwa ukaribu zaidi.

Aidha wajumbe hao wakaeleza namna mafunzo ya mguso waliyopatiwa na shirika la Uzikwasa yanavyoendelea kuwasaidia katika shughuli zao za kila siku.
Katika hatua nyingine kufuatia baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo kutokuwa na mahudhurio yanayoridhisha, katibu msaidizi wa kamati ya VMAC Kimang’a Daudi Bushishi, ameeleza mpango uliopo usoni, ambao utatangaza nafasi mbili zitakazoachwa wazi ili kujazwa.

Haya yote yanajiri kufuatia shirika la uzikwasa, kuwa na mafunzo saidizi yanayolenga kuzitembelea kamati za kudhibiti ukimwi jinsia na uongozi vmac za vijiji wilayani Pangani, hasa kwa viongozi waliopatiwa elimu ya mguso.

No comments

Powered by Blogger.