AFISA USHIRIKA, NMB PANGANI WAKUTANA NA WANACHAMA WA SACCOS
Suala la elimu ya ushirika na usimamizi wa fedha kwa
wajumbe wa bodi na wanachama wa chama cha ushirika Mwera na Sakura Estate
wilayani Pangani, limeonekana kuwa chini hali iliyosababisha baadhi ya
wanachama hao kushindwa kufanya kazi zao kulingana na taratibu za ushirika.
Hayo yameelezwa na Afisa ushirika wilayani Pangani Bwana
Julius Chagama katika mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika katika kijiji cha
Mwera kwa kuwashirikisha benki ya NMB tawi la Pangani, ambapo amesisitiza kuwa
elimu ya ushirika na usimamizi ni muhimu
kwani ndiyo inayomsaidia mwanachama na mjumbe wa bodi katika kuweka akiba.
“Ndio maana bado tunasisitiza kwamba elimu ya
ushirika ni muhimu kwa mujibu wa sheria, na wakati wowote ukiangalia sheria
zetu hata ukianzia huko nyuma zilikuwa zinatenga asilimia ishirini na tano ya
ziada inayopatikana kwa mwaka kwaajili ya elimu, elimu haiishii kwenye mkutano
mkuu tu kama wanachama naona hapa wanaelewa hivyo, kuna elimu kwa viongozi wa bodi lakini kupitia
kwenye kamati zao kama vile kamati za mikopo kamati ya usimamizi lakini pia
kuna elimu ya watendaji.”Amesema Bwana Chagama.
Kwa upande wake aliyekuwa mwenyekiti wa bodi hiyo
kwa awamu iliyopita Bwana Kibaden
Laurian amesema baada ya kupata elimu ya ushirika, baadhi ya watu wamepata muamko na kujua
umuhimu wa kuweka akiba tofauti na awali.
“Wakati tunaanza wengi walikuwa hawajui ushirika
lakini baada ya kupata sasa semina kutoka kwa mrajisi wa wilaya Bwana Chagama
baadhi wameweza kupata mwamko na kuendelea kijiunga zaidi na kuelewa umuhimu wa
kuweka akiba, kwa sababu wengi wamekuwa na mawazo kwamba kipato wanachokipata
ni kidogo kwa hiyo hana uwezo wa kuweka pesa nyingine kwenye mfuko wa saccos ili aweze kukopa ili
aweze kupata pesa ya kutosha ili aweze kufanya shughuli nyingine, kwa hiyo
inaonyesha kwamba elimu sasa kadri tunavyoendelea kipindi tulichokuwepo
tumejitahidi kadri ya uwezo wetu mimi mwenyekiti pamoja na bodi yangu kwa
ujumla” Amesema Bwana Kibaden.
Abel Chitojo ni meneja wa tawi la NMB Pangani ambaye
ni mgeni rasmi kwenye mkutano huo amesema kuwa kutokana na wanachama walio
wengi kutokuwa na uelewa juu ya elimu ya kifedha wataendelea kutoa elimu hiyo na pia
kuendeleza ushirikiano baina yao.
“Tutaendeleza ushirikiano na saccos ya Mwera na
Sakura Estate kwani ni wateja wetu, pia kuendelea kuwapatia elimu ya kifedha
hasa wanachama wake wa Mwera ambao mnajua wengi ni wafanyakazi na vibarua
wadogo wadogo, kwa ajili ya kuweza kupata ule uelewa wa fedha, unajua kuna watu
wanapata fedha lakini matumizi ni kama vile akipata mshahara wote unaisia
kwenye chakula tu, pia kuweza kuweka na kukopa, jinsi gani unaweza kupata
faida”Amesema Bwana Abel
Nao wanachama waliojiunga na chama hicho wameelezea
mafanikio waliyoyapata, huku wakiwashauri wengine kutokuwa wazito kujiunga na
chama hicho.
“Wengi elimu inawaingia kutokana maendelieo madogo
madogo ambayo wenzao wanaona na wanayapata, mimi mwenyewe nikiwa mwanachama na
ni mjumbe naweza kusema kwamba saccos ndio imeniwezesha kwamba hadi leo
najivuna nawezasema kuwa nina nyumba nzuri ya thamani, nawashauri tusiwe wazito
kujiunga. Tangu tulivyoanza kwenye saccos yetu mimi nilikuwa siwezi kumiliki
milioni hata mbili lakini kwa sasa namiliki zaidi ya nne” Amesema mjumbe mmoja.
Hayo yamejiri kwenye Mkutano mkuu wa chama cha
ushirika Mwera wa kujadili masuala mbalimbali ya chama hicho na miongoni mwa wananachama
hao ni kutoka Chama cha ushirika Mwera, Sakura, na Kigombe Estate na Tanga
kilichoanza mwaka 2002.
Mbali na mkutano huo pia Benki ya NMB tawi la
Pangani ilipata nafasi ya kuelimisha wanachama hao kujiunga na benki hiyo na kufanikiwa
kuwafungulia akaunti baadhi ya wanachama ambao hawakuwa wanatumia huduma hiyo.
No comments