PANGANI YAZINDUA RASMI WIKI YA MAJI DUNIANI LEO
Uzinduzi wa wiki ya maji kitaifa umetangazwa rasmi
leo ambapo katika Wilaya ya Pangani imeelezwa kuwa juhudi za makusudi za
utunzaji wa mazingira kwa ujumla, zinahitajika ili kufanikisha upatikanaji wa maji
safi na salama hasa katika maeneo ya mjini na vijijini.
Akizungumza kwenye kipindi cha ASUBUHI YA LEO
kinachorushwa na kituo hiki Mhandisi wa Maji kutoka Halmashauri ya Wilaya ya
Pangani Bwana Novat Wilson, amesema kuwa katika kuadhimisha wiki ya maji wamejipanga
kutoa elimu kupitia kituo cha redio Pangani Fm ili kuikumbusha jamii jukumu lao
katika kuhifadhi vyanzo vya maji.
“Ni vizuri kwamba leo kupitia Radio hii tuzungumze
na wananchi katika maadhimisho haya ya wiki ya maji ambayo yapo kila mwaka
mwezi machi tarehe 16 hadi 22, tunatoa elimu ya kuwakumbusha na kuwahamasisha
wanajamii kujua wajibu gani wanapaswa kuchukua kuhusu uhifadhi na utunzaji wa
vyanzo vya maji” Amesema Mhandisi Novat na kuongeza kuwa.
“Kwa wiki nzima kuna miradi tumepanga kuitembelea kuangalia
inaendeleaje, ila pia kuendelea kuhamasisha wananchi kuhifadhi vyanzo vya maji
wanavyovitumia. Na kuanzia kesho tarehe 17 ya mwezi huu wa Machi tutafika
kijiji cha Mzambarauni ambacho mradi wake ulitekelezwa katika awamu ya kwanza ya
utekelezaji wa maji safi vijijini, pia tutatembelea mradi wa maji wa Bweni ambapo
tutakuwa na zoezi kama hilo, na tarehe 19 tutakuwa kijiji cha Mseko kwa sababu
tumekuwa na changamoto ya maji kwa muda mrefu”Amesisitiza Bwana Novat.
Aidha Mhandisi huyo wa Maji amezungumzia hali ya
upatikanaji wa maji safi na salama wilayani Pangani akisema bado kuna
changamoto kutokana na miundombinu iliyopo kutoendana na uhalisia wa sasa, na
kuongeza kuwa ili kulinda afya za watumiaji wa huduma hiyo ni muhimu kutibu
maji hayo kuwa safi na salama kabla ya kuwafikia wananchi kwa ajili ya
matumizi.
“Kwa
ujumla hali ya upatikanaji wa maji Pangani niseme ipo kati si chini sana wala
si kwamba ipo juu sana, kwamba upande wa maji safi na salama tunachangamnoto,
lazima tuwaambie watu kwamba tuna changamoto kwa sababu miradi mingine
iliyofanyika zamani haikuzingatia zile standard za maji kwa sababu unakuta
mradi umejengwa lakini una’Pump maji moja kwa moja kwenye mto unapeleka kwenye
matumizi ya watu jambo ambalo sio zuri” Amesema Mhadisi wa maji Wilaya ya
Pangani.
Na kusisitiza …. “Kwahiyo sasa serikali
inachokifanya katika utekelezaji wa miradi ya maji safi na salama vijijini, kwamba
watu inabidi wafahamishwe jinsi ya kutibu maji yaweze kuwa safi na salama kwa ajili
ya matumizi kwa kuhakikisha kwanza yanachujwa na baada ya hapo yanatibiwa kabla
ya kuingia kwenye matumizi”.
Mhandisi huyo wa maji Pangani, pia amekiri usugu wa
changamoto za upatikanaji wa huduma hiyo katika baadhi ya vijiji wilayani humo
ikiwemo kijiji cha Meka, Mseko na Masaika, na kusema kuwa mikakati yao ni
kuhakikisha hadi kilele cha wiki ya maji Machi 22 mwaka huu wanawaacha salama
wananchi hao wakipata maji ya uhakika kwa matumizi.
(Watangazaji wa Pangani Fm kuanzia kushoto ni Hamisi Makungu pamoja na Kelvin Mpinga wakisikiliza kwa makini wakati wakifanya mahojiano na Mhandisi Novat Wilson katika studio za Pangani Fm kwenye kipindi cha Asubuhi Ya Leo)
“Ni kweli kwamba tumekuwa tunachangamoto ya maji
katika baadhi ya miradi, kuna changamoto nyingine ambazo zimekuwa za muda mrefu
lakini sisi tunakabiliananazo na zinaisha. Sasa kwa kijiji cha Mseko tunaimani
kabla ya kilele cha wiki ya maji basi watakuwa wamerejeshewa maji angalau hii
wiki inapoisha, wenyewe waseme kweli wiki ya maji imewaacha salama”. Amesema
Bwana Novat Wilson.
Ameongeza kuwa.. “Kuhusu Masaika ni kijiji ambacho
kilikuwa katika awamu ya kwanza ya kupatiwa miradi ya maji safi na salama
vijijini ambayo ilianza mwaka 2006/2007, lakini shida iliyopo hapo ni kwamba
visima vya pale kila kunapochimbwa maji hayapatikani kiasi cha kutosha kwa hiyo
ule mradi haukuweza kukamilika kwenye awamu ya kwanza kutokana na kukosa chanzo
cha maji cha chini ya ardhi.
Amesema… “Na katika wamu ya pili, pia tuliwachimbia
kisima chenye urefu wa mita 100 ila pia kisima hicho kikawa na changamoto hiyo hiyo,
kwa hiyo sasa njia mbadala ambayo tunaona inaweza ikafaa, ni kuwaweka kwenye
mpango wa kuvuna maji kupitia mabwawa yaliyopo pale ambayo tukiyaboresha vizuri,
yale maji tukiyachuja na kuyatibu yanaweza yakawa maji mazuri tu kwao” Amesema
Mhandisi huyo.
Maadhimisho ya Wiki ya Maji kitaifa na kimataifa
yanayofanyika kila mwaka ifikapo tarehe 16 hadi 22, na mwaka huu wa 2018
yamebeba kauli mbiu isemayo “Hifadhi maji na Mfumo wa Ikolojia kwa maendeleo ya
Jamii”, ambapo kwa wilaya ya Pangani kilele cha maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika
katika kijiji cha Boza Wilayani humo.
No comments