FAHAMU KWA UNDANI LISHE YA MTOTO KATIKA MAKUZI YAKE



Unyonyeshaji wa mtoto unaozingatia maelekezo na taratibu zinazoelezwa na wataalam wa Afya kuanzia anapozaliwa hadi anapofikisha miaka miwili, umeleezwa kuwa ni muhimu katika makuzi bora ya mtoto kiakili na hata kimwili.

Akizungumza kwenye kipindi cha ASUBUHI YA LEO kinachorushwa na kituo hiki Kaimu Afisa Lishe kutokea Wilayani Pangani Daktari Bahati Issa, amesema kuwa pasi na kuangalia mtoto amezaliwa kwa njia gani, ni muhimu kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee katika kipindi chote cha miezi sita ya mwanzo, bila kulishwa chakula kingine chochote.

“Mama anatakiwa amnyonyeshe mtoto wake ndani ya dakika thelathini mpaka saa moja baada ya kujifungua kama huyo mama amejifungua kwa njjia ya kawaida, na kama amejifungua kwa njia ya upasuaji baada ya saa tatu hadi nne anatakiwa awe ameanza kumnyonyesha mtoto” Amesema Dk Bahati na kuongeza kuwa...

“Kwa muda wa miezi sita mtoto anatakiwa anyonyeshwe maziwa ya mama pekee, asipewe chakula chochote kwani maziwa ya mama yana kila hitaji la mtoto katika umri ule hadi atakapotimiza miezi sita ya mwanzo, kuna faida za kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama pekee kwa kipindi hicho, faida hizo ni kwamba maziwa ya mama yanapatikana muda wote na hayana gharama, maziwa yanavirutubisho vya kutia nguvu, kutia joto, kujenga mwili na kulinda mwili, vilevile maziwa ya mama yana kiasi cha maji kulingana na umri na hitaji la mtoto, ni kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali, yanavirutubisho vinavyosaidia ukuaji wa mfumo wa fahamu wa mtoto, pia hujenga urafiki kati ya mama na mtoto na kingine unyonyeshaji hupunguza uwezekano wa kupata saratani ya matiti na kizazi” Amesisitiza Dokta Bahati.




Aidha Daktari Bahati ameeleza kuwa, kitaalam mtoto anatakiwa achanganyiwe vyakula vingine mbali na maziwa ya mama anapofikisha umri wa mizezi sita ya mwanzo tangu kuzaliwa, na kuongeza kuwa katika kipindi hicho vyakula anavyopaswa kupewa ni vile vitakavyoendelea kumsaidia katika ukuaji wake.

“Mtoto anapotimiza miezi sita ni kipindi ambacho unahitajika kumuongezea chakula cha ziada huku akiendelea kunyonya maziwa ya mama mpaka miaka miwili au zaidi. Maziwa ya mama pekee hayatoshi kumpatia mtoto virutubisho vyote kwaajili ya ukuaji wake, pia mtoto huyu anakuwa ameshakuwa mkubwa kwa hiyo jinsi mtoto anavyokua ndivyo kiasi cha chakula kinatakiwa kiongezwe kufikia mahitaji yake ya lishe kwa ajili ya ukuaji zaidi” Amesema Dokta Bahati na kuongeza kuwa…

“Vyakula ambavyo anatakiwa amtoto apewe kwa kipindi hiki, ni ule mchanganyiko wa makundi yote sita ya chakula, vyakula hivi ni Carbohydrate, hivi ni vyakula vya wanga vinavyotia nguvu mwilini-  mfano uji wa nafaka kama Mahindi, Mtama, Mchele, Ngano, Viazi hili ni kundi moja, kundi jingine ni vyakula vya Protein hivi ni vyakula vya kujenga mwili kwa mfano Karanga, Maharage, Soya, Maziwa na Mayai”. Ameyataja makundi mengine kuwa ni…

“Kuna kundi la vyakula vya kutia nguvu na joto mwilini, kwa mfano mafuta ya mimea ikiwemo mafuta ya Kweme, mafuta ya Alizeti, Mzaituni, mafuta ya Nazi na mafuta ya kwenye maziwa pia mafuta ya Samaki. Kundi la nne ni Vitamin na kundi la tano ni Madini hapa huyu mtoto kwenye chakula chake anatakiwa aekewe mbogamboga na matunda, kama vile Karoti, Boga, Ndizi, Apple, na Matikiti na kundi la sita ni maji ambayo kwa kipindi chote tangu azaliwe mtoto huyo hajapewa maji, kwa hiyo baada ya kutimiza miezi sita anaweza kuanza kupewa maji kwa sababu mtoto huyu tumeshaanza kumchanganyia vyakula vingine”. 



Ameongeza kuwa mchanganyiko huo wa vyakula ni muhimu pia iwapo utazingatiwa utaratibu unaoelekezwa na wataalam, utamuepusha mtoto na magonjwa kama ya utapiamlo kutokana na kukosekana kwa utaratibu mzuri wa lishe.

“Chakula kinatakiwa kiandaliwe katika mazingira safi na salama, kisiwe na vitu vigumu kama vifupa au mbegu mbegu, ni muhimu kutochanganya vyakula vingi kwa wakati mmoja kwa sababu mtoto anaweza kupata aleji ukashindwa kujua nini kimemsababishia hiyo aleji, kwa hiyo unatakiwa wakati unaanza kumlikiza huyu mtoto uwe unaanza chakula kimoja kimoja, kwa sababu mtoto huyu wa miezi sita pia anatakiwa anyonye kwanza kabla ya kupewa chakula cha ziada”Amesema Dk Bahati na kuongeza kuwa... 

“Vyakula vya ziada anatakiwa apewe mara mbili au mara tatu kwa siku na visizidi vijiko vitatu vya chaklula kwa siku, na vyakula vya mtoto vyote huwa vinachemshwa na havitiwi viungo vyovyote”.

Ameongeza kuwa “Mtoto wa miezi 7-8 anaweza kupewa mchanganyiko wa makundi yote ya chakula katika mchanganyiko uliopondwa baada ya kunyonya maziwa ya mama, ambapo anatakiwa apewe chakula cha ziada mara mbili hadi tatu kwa siku kwa idadi ya vijiko vitatu hadi tisa kwa siku. Pia mtoto wa miezi 8 anapenda kushika mwenyewe, hivyo unaweza kumpa vyakula vya kushika kama Maandazi, Chapati akawa anashika huku anakula mwenyewe” Amesema Dokta Bahati na kuongeza kuwa…



“Sasa tuje mtoto wa miezi 9-12 umri huu mtoto huwa na meno pia huwa anafahamu ladha ya chakula mbalimbali, hivyo unaweza kumlisha vipande vidogo vidogo vya chakula kigumu au vyakula laini vilivyopondwa, umri huu mtoto anaweza kupewa milo mitatu hadi minne ya chakula kwa siku.

Kama mtoto anaweza kula kwa mikono yake ni vizuri kumuacha pia kujizoesha kuchukua vitu na kula. Na umri wa miezi 12-24 yaani miaka miwili, umri huu mara nyingi mtoto anakuwa anatembea, anaanza kuongea na pengine wakati mwingine analazimisha hata kula mwenyewe, ni umri unaoweza kuanza kumpa vipande vidogo vya chakula hata vyakula vinavyoliwa na familia, na apewe milo mitatu mpaka mitano kwa siku” Amesema Dokta Bahati.


Sanjari na hayo Kaimu Afisa Lishe Wilayani Pangani Daktari Bahati Issa, amesema kuwa ulishaji mbovu wa mtoto usiozingatia maelekezo ya wataalam, kunaweza kusababisha udumavu wa mtoto kiakili na hata kimwili.

“Ulishaji mbaya wa mtoto ndio unatuletea watu sasa hivi, unaona vijana wengi unamwambia fanya hivi hafanyi, yani wapo tu kwenye kazi za kawaida kawaida, kwahiyo kama mama yake au familia yake ingeweza kumlisha vizuri kama inavyotakiwa huyu mtoto angekuwa vizuri na ndo zile A za darasani la kinyume chake ndo yale masifuri mengi ambayo sasa hivi tunahangaika nayo na mwisho tunapata viongozi wabovu na wenye maamuzi mabovu” Amemalizia Dokta Bahati. 

Amemalizia kwa kuwataka wazazi kuzingatia lishe zao katika siku elfu moja, kabla ya kupata ujauzito, kipindi cha ujauzito na baada ya kujifungua, akisema siku hizo ndio mustakabali wa mtoto katika maisha yake yote.

2 comments:

Powered by Blogger.