PANGANI NZIMA SASA KUPATA UMEME
Serikali inatarajia kukamilisha zoezi la kusambaza umeme katika
vijiji na maeneo yote wilayani Pangani
ndani ya mwaka huu wa 2018 ili kuboresha maisha ya wananchi kwa upande wa nishati kupitia mradi
wa REA awamu ya tatu.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nishati Mheshimiwa Dkt.
Medard Kalemani wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mivumoni wilayani
humo katika ziara yake ya hivi karibuni na kusema kuwa wao kama serikali wanayo
matumaini ya kuwa mradi huo utatekelezwa na kukamilishwa ndani ya mwaka huu katika vijiji na vitongoji
vyote ambavyo havina umeme wilayani Pangani japokuwa wamempa mkandarasi miezi
ishirini na nne kukamilisha kazi ya kusambaza umeme wilaya nzima.
“Tumetekeleza miradi mitatu hapa Pangani kati ya vijiji 33 vilivyokuwa ndani ya wilaya yetu bado ni
vijiji vitano havijapatiwa umeme, bado vitongoji vingi havijapata umeme.
Msaraza ambako bado, Mtonga ambako bado, na Mtango, Bado wananchi wengi
hamjaunga umeme tumemleta mkandarasi huyu tumempa miezi takribani ishirini na nne
kukamilisha kazi katika wilaya nzima ya Pangani na bahati nzuri ana maeneo
machache ni vijiji vitano tu na vitongoji kumi na moja tuna matumaini ndani ya
mwaka huu atakamilisha mapema iwezekanavyo.” Alisema Mh.eshimiwa Kalemani.
Aidha Mheshimiwa Kalemani amesema baada ya vijiji vyote
kukamilika kusambaziwa umeme mkandarasi atafanya kazi ya kurudia katika sehemu
ambazo zimerukwa ili kuifanya Pangani sehemu ya mfano katika upatikanaji wa
Nishati ya umeme na kuvutia wawekezaji kujenga viwanda.
Mheshimiwa Waziri Kalemani amewataka wakazi wa Pangani kuwa,
mradi utakapokamilika kuitunza miundombinu yake ili iweze kudumu kwa mrefu huku
akiwasisitiza kuchangamkia fursa mapema ya kuunganishiwa huduma hiyo kwa kuwa endapo mradi ukiwa tayari gharama ya kuunganishiwa
umeme itakuwa ni kubwa.
“tutunze miundombinu ya umeme inayokuja, nguzo hii ikiwekwa
mtu mmoja akaikata watu zaidi ya arobaini watakosa umeme kwa mkupuo, transforma
ikifungwa mtu akaiba mafuta wananchi zaidi ya mia moja watakosa umeme kwa
mkupuo hivyo tutaanza kulalamika, kwahiyo niwaombe tuitunze miundombinu ili na
sisi itutunze. Na wananchi ambao watachelewa muda ukaisha mradi ukapita
mtaingia gharama kubwa ya kuunganisha umeme kwahiyo mimi niwaombe kabisa
waheshimiwa wenyeviti wa vijiji na viongozi wengine tuwahamasishe wananchi
hawa” Alisema Mheshimiwa Waziri.
Waziri huyo wa Nishati pia amewashauri wananchi wenye vyumba
vichache kutoingia gharama ya kufanya wiring
katika nyumba zao na badala yake watumie kifaa maalumu kinachoitwa UMETA kwa
ajili ya kuepusha gharama ambapo wateja 200 wa mwanzo hadi 250 watapatiwa bure na
tayari wazee watano wa kijiji cha Mivumoni wameshapatiwa vifaa hivyo bila ya
malipo.
“Wananchi ambao uwezo wenu ni mdogo ambao hamjavuka hatua,
kama nyumba yako ina chumba kimoja, viwili, vitatu hadi vinne msihangaike
kuingia gharama ya kufunga wiring tumieni
kifaa hiki kinaitwa UMETA ukiwa na chombo hiki una umeme tayari, chombo hiki
kinatolewa bure kwa wateja wa mwanzo 200 hadi 250, ukiwa na chombo hiki
utaunganisha umeme wake na Friji, Jiko la umeme, na utaunganisha na TV wale
vijana wenzangu utaangalia mpira wa Manchester na Arsenal mjini, sasa unakwenda
kufanyako nini? “ Alisisitiza Mheshimiwa Medard Kalemani.
“Kama umeme unakatika ni kwa sababu ya miundombinu na kwa
bahati mbaya kuanza Majani Mapana hadi Pangani kuna miti mingi kwa hiyo
ikitokea upepo popote pale mti ukagusa nyaya lazima utayumba na kukatika sasa
tunachokifanya ni kufanya survey, na
tunataka kujenga substation mpya huku
Pangani ambayo itakuwa inafua umeme huku huku ili kupunguza umbali mrefu hiyo
ndiyo itakuwa ni jitihada kubwa tutakuwa na suluhisho la kudumu vinginevyo
kutokana na mabadiliko haya ya hali ya hewa yataendelea kutusumbua lakini mkakati
wa kuhakikisha kwamba umeme unakuwa imara katika wilaya ya Pangani ni jambo
ambalo tumeanza kulifanyia kazi.” Alisema Mheshimiwa Medard Kalemani.
Wakati wote wa ziara yake wilayani Pangani Mheshimiwa Waziri
wa Nishati Medard Kalemani aliambatana na Mkuu wa wilaya hiyo Bi Zainab
Abdallah Issa, aliyekuwa Mkurugeniz wa halmashauri ya Pangani aliyesimamishwa
kazi hivi karibuni Bwana Sabas Damian Chambasi, pamoja na viongozi wengine wa
serikali na chama kutokea wilayani Pangani.
(Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mivumoni wakifatilia kwa makini wakati Mheshimiwa Waziri wa Nishati Dkt.
Medard Kalemani alipokuwa akizungumza nao)
Ziara ya Mheshimiwa waziri huyo wa Nishati ambayo ilianzia
katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Pangani ilikuwa na lengo la kukagua
utekelezaji wa mradi wa REA awamu ya pili na tatu ikiwa ni pamoja na kujua
changamoto za nishati katika mkoa wa Tanga kwa ujumla.
No comments