JESHI LA POLISI PANGANI LATOA SHUKRANI KWA WANANCHI KATIKA KUFANIKISHA KUZIMA MOTO

Jeshi la Polisi wilayani Pangani limetoa shukrani kwa wananchi
waliojitokeza kushiriki katika kuuzima moto uliozua taharuki katika
eneo la kiwanda cha kuchakata Makumbi kilichopo eneo la Funguni
wilatani Pangani.
Akizungumza na Pangani FM mara baada ya kuudhibiti moto huo,
kamanda wa Polisi wilayani humo Bi Christina Musyani amesema kuwa
wananchi wamefanya jitihada kubwa katika kuuzuia na kuudhibiti moto
huo kwa kushirikiana na kikosi cha zima moto.

"Tunashukuru sana wananchi wa Funguni kwa ushirikiano waliotoa
katika kuudhibiti moto huu kulingana na uwezo wao, lakini pia
tuliwasiliana na kikosi cha zima moto ambacho bado kipo mpaka sasa"
alisema Kamanda Musyani.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Pangani Bi Zainabu Abdallah Issa ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani humo ametoa pole kwa mwekezaji wa kiwanda hicho pamoja na wananchi wa eneo la Funguni kwa tukio hilo  huku akiwataka wananchi kuwa na subira hasa kwa wakati huu.

"Kwanza kabisa nitoe pole kwa wananchi wote wa Pangani hususani
wakazi wa eneo hili kwa tukio hili la moto lililotokea hapa kwenye kiwanda cha Makumbi, jitihada zimefanyika lakini kama mnavyojua
hali ya makumbi yanaposhika moto, viongozi wote wa wilaya tupo hapa
kuhakikisha usalama unakuwepo, na pia tushatoa taarifa mkoani"
alisema Mkuu wa wilaya.

Inaelezwa kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme iliyojitokeza majira ya asubuhi katika eneo hilo la kiwanda, lakini mpaka sasa tayari serikali kwa kushirikiana na wananchi wameshaudhibiti moto huo.

No comments

Powered by Blogger.