AWESSO AMSHUKIA MWEKEZAJI WA AMBONI PLANTATION KWA KUTOTII MAAGIZO YA SERIKALI
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mheshimiwa JUMAA
AWESSO ameahidi kumchukulia hatua Mwekezaji wa shamba la Mkonge la Amboni Plantation
Bwana Hugo Johnson kwa kutotii maagizo ya serikali.
Hayo yamejiri katika ziara ya siku mbili ya Naibu Waziri
huyo ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Pangani wakati akizungumza na wananchi wa
kijiji cha Mwera na kusema kuwa mwekezaji huyo ameshindwa kutekeleza agizo
lililotolewa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mheshimiwa SULEIMANI JAFFO alilolitoa mwaka jana
lililomtaka kumalizia ujenzi wa chumba cha upasuaji kwa wakina mama katika
kituo cha afya cha Mwera.
‘’Kuhusu ujenzi huu wa kituo cha afya pamoja na
nguvu za wananchi lakini Mheshimiwa Suleimani Jaffo ameagiza muwekezaji wa eneo
hili amalizie ujenzi huu, Mheshimiwa mkuu wa Wilaya mpaka sasa hivi mwekezaji
yule amekaidi, amekataa, na ameona kwamba hakuna mtu yeyote atakayefanya jambo
lolote hiyo ni aibu kubwa sana hususani kwa wilaya yetu ya Pangani, zipo faida
ambazo wananchi wanatakiwa wanufaike nazo kutokana na mwekezaji kama vile Afya
, Elimu, Maji na kama kuna Miundombinu mibovu ya Barabara basi aborshe ili
wananchi waweze kunufaika’’ Asema Mheshimiwa Awesso.
Ameongeza kwa kuwataka wawekezaji kutatua kero za
wananchi wa eneo husika na sio kujinufaisha wenyewe kutokana na uwekezaji.
“Laiti kama wawekezaji wetu wa wilaya ya Pangani
kama wanatusaidia hata kisima kimoja kimoja basi wilaya yetu isingekuwa na
shida ya maji, hivi kweli anashindwa kutupa sisi mchanga, anashindwa kuchangia kitu cha maendeleo ambacho hata wafanyakazi
wake katika zao la Mkonge watapata huduma? Mheshimiwa mkuu wa wilaya mnyonge
mnyongeni haki yake mpeni kwa sisi tufikie hatua ya kuwasaidia wananchi
wetu’’Alisema Awesso.
Naibu Waziri huyo wa Maji na Umwagiliaji alifanya
ziara ya siku mbili katika jimbo lake la Pangani kwa ajili ya kukagua miradi
mbalimbali ya kimaendeleo ili kujipanga kuelekea Bungeni mnamo mwezi ujao.
No comments