CHANGAMOTO YA MAJI BADO KITENDAWILI KWA WAKAZI WA MASAIKA WILAYANI PANGANI
Wananchi wa kata ya Masaika wilayani Pangani wameiomba
serikali hususani halmashauri ya wilaya kuweka jitihada katika ufanikishaji na upatikanaji
wa maji safi na salama kutokana na adha wanayokutana nayo kwa sasa.
Wakizungumza na Pangani Fm baadhi ya wananchi wa
kijiji cha Masaika Mlimani wamesema kuwa hali ya upatikanaji wa maji katika eneo
lao sio nzuri kutokana na kisima kilichokuwepo hakikidhi huduma ya maji kwa
kila kaya jambo linalowalazimu kujiwekea idadi ya ndoo tatu kwa kila nyumba.
“Masaika bado suala la maji linasumbua ni gumu
pamoja na jitihada zinazofanyika za uchimbaji wa visima lakini bado visima
hatujafikia kuwa navyo kabisa, na tunatafuta maji kwa foleni, mtu unaamka
kuanzia saa kumi za usiku na kurudi nyumbani saa mbili au saa tatu asubuhi, kwa
kweli sisi kina mama tunapata shida sana.’’ Amesema mama mmoja
aliyejitambulisha kwa jina la Hidaya.
Bi Amina Awadhi ni mjumbe aliyechaguliwa na kamati
ya kusimamia uchimbaji wa visima vya maji katoka katika kijiji cha Masaika Mlimani
kwa upande wa wananchi, ametumia nafasi hii kuwaomba wataalamu wa maji na
wachimbaji visima katika kata ya Masaika kuzingatia kukutana na wenyeji kabla
ya utafiti wa uchimbaji.
“Mimi kama
mmoja kati ya wananchi niliyechaguliwa na kamati, niwaombe serikali pamoja na
injinia wa maji kipindi watakachokuja Masaika kutuchimbia visima ni vyema
wakakutana na wenyeji wa hapa ili tuwaonyeshe sehemu sahihi ambayo watapata
maji’’ Bi Amina.
Bwana Michael Richard nae ni afisa mtendaji wa kata
ya Masaika, amesema kwa sasa mpango uliopo kwa wanakijiji wa eneo hilo ni
kuzifufua sehemu ambazo zina uwezekano wa kupata maji ili kuleta nafuu kwa
wananchi hao.
‘’Mpango wetu kama kijiji ni kuzifufua sehemu ambazo
zina uwezekano wa kupata maji na kuna bomba pia tutalifufua, wakazi wa Masaika
wanapata shida na hata maji wanayoyatumia ni ya Bwawa na hutumiwa sana na
wanyama hivyo si safi na salama’’ Amesema Bwana Michael.
Kwa upande wake Mhandisi wa maji kutoka halmashauri
ya wilaya ya Pangani Bwana Novat Wilson amekiri kuwepo kwa changamoto ya
upatikanaji wa maji eneo la Masaika, huku akieleza mpango mkakati uliopo wa kufanya
utafiti utakaopelekea kuweka miundombinu mizuri ya upatikanaji wa maji safi na
salama.
“Mipango yetu kama serikali ni kulifanyia
matengenezo Bwawa lililopo hepo eneo la Masaika na tutalitumia katika uvunaji
wa maji ya mvua na naamini tukiliwekea miundombinu mizuri wananchi watanufaika
na Bwawa hilo’’ Amesema Mhandisi wa maji Bwana Novat.
Ameongeza kuwa…‘’Matarajio yetu kwa Masaika baada ya
zoezi la usanifu wa hilo Bwawa tumeziweka katika mikakati ya mwaka wa fedha
2018/2019 kwa hiyo tumeiweka bajeti hiyo ili ifikapo mwezi wa sita mwaka huu huenda
tukapata hizo fedha kwa ajili ya matengenezo.
No comments