MKANDARASI MSAIDIZI MBARONI KWA KUSUA SUA KWA MRADI WA MAJI PANGANI
Mkandarasi msaidizi wa kampuni ya KHARTON TRADERS
LTD Bwana DIKANZA AMIRI MWAYA amekamatwa na kuwekwa ndani na jeshi la polisi
wilayani Pangani kutokana na agizo lililotolewa na Naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji
nchini Mheshimiwa Jumaa Hamidu Awesso baada ya kutoridhishwa na ujenzi wa mradi
wa maji katika kijiji cha Mtango wilayani Pangani.
Hayo yamejiri wakati wa ziara ya kukagua miradi mbalimbali
ya Maendeleo katika wilaya hiyo ambapo Naibu Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa
Pangani alipata nafasi ya kutembelea ujenzi huo katika kijiji cha Mtango, Kata
ya Mikinguni ili kuona maendeleo ya mradi lakini alishangazwa kuona ukisuasua
ambapo aliagiza kusimamishwa kwa ujenzi katika eneo hilo.
Akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Pangani Mheshimiwa
Zainab Abdallah Issa, Mkurugenzi wa Halashauri ya Wilaya ya Pangani Bwana Sabas
Damian Chambasi na viongozi wengine kutoka halmashauri hiyo, Mheshimiwa Awesso alimweleza
mkandarasi msaidizi wa kampuni ya KHARTON TRADERS LTD Bwana Dikanza Amiri Mwaya
ya kuwa;
“Hakuna kitu ninachokifuatilia kama huu mradi,
nataka uelewe tu na nikueleze kwamza huu mradi ulikuwa unasua sua na hatutasita
kuwanyang’anya kama hamko tayari na hamtafanya kazi yenu vizuri kwa sababu sisi
kama wizara hatukuwa kikwazo katika kuwalipa pesa zenu, Mkurugenzi nikuambie tu
zipo taarifa katika huu mradi kuna baadhi ya vifaa vinauzwa kama ulikuwa hujui,
msije mkauza vifaa na mradi ukatoka wa ajabu ajabu hatuta kubali kubambikiwa, na
kama mtafanya kazi kiujanja ujanja hamtalipwa’’ Alisema Mheshimiwa Awesso
Katika hatua nyingine suala la kutokuwepo kwa
mkandarasi mkuu wa ujenzi wa mradi huo ambaye alimtuma mwakilishi wake na hivyo
kuonekana kutoa ya kubabaisha, lilionekana kumkera Mheshimiwa Awesso na kuagiza
mkandarasi mkuu Bwana Karim Mohamed Jiwa kumfuata mkoani DODOMA kwa ajili ya
mazungumzo zaidi, lakini badae akiwa kwenye mahojiano na kituo cha redio
Pangani FM, alibadili uamuzi huo na kumtaka mkandarasi huyo kufika kwa Mkuu wa
Wilaya Zainab Abdallah Issa na ndipo aende Dodoma.
Akizugnumza kwenye mahojiano maalumu kwenye kituo
cha redio Pangani Fm, Mheshimiwa Jumaa Awesso alimtaka Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Pangani Bwana Sabasi Damiani Chambasi kuwa makini na kitengo cha
manunuzi kwa kuhakikisha anawapa tenda watu sahihi watakaofanya kazi kwa
ufanisi.
“Kikubwa Mkurugenzi kuna jambo kubwa sana hapa limejificha,
cha kujifunza angalia vizuri kitengo chako cha manunuzi tuwape watu wenye uwezo, na wanaotoa tenda sio mtu ametoa
asilimia fulani ya pesa kwa sababu ni sehemu na yeye anatakiwa apate wananchi
wa Mtango wanapata tabu, mimi nataka niwahakikishie kama huu mradi hautaeleweka,
hakuna mtu atakayelipwa fedha hakuna atakayepata fedha, kwa nini hayupo eneo la
kazi mpaka muda huu na kwa nini katuma mwakilishi si kwa sababu kajua mradi
hauna kiwango na una kasoro, Mkurugenzi usilale fedha nyingi sana zimetumwa kwa
ajili ya mradi huu kama hauta fanya vizuri msimamo wangu upo pale pale hakuna
mtu atalipwa fedha, haiwezekani kutekeleza mradi kiujanja ujanja.’’ Amemalizia Mheshimiwa
Awesso
Takribani shilingi milioni mia tano (500) zilitengwa
kwa ajili ya Ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Mtango, ambapo mpaka
sasa Mkandarasi aliyetajwa kwa jina la Karim Mohamed Jiwa kupitia kampuni ya
Kharton Traders, ambayo ina usajili wa bodi ya wakandarasi nchini (CRB) kwa
namba B6/0591/11/2011, huku ikipewa daraja la sita (6) ameshalipwa shilingi
milioni sabini na mbili (72), lakini mpaka sasa mradi bado una suasua.
No comments