WANANCHI PANGANI WATAKIWA KUTOA USHIRIKIANO KWENYE VYOMBO VYA SHERIA


Wananchi wametakiwa kutoa ushirikiano kwenye vyombo vya sheria hasa katika suala la kutoa ushahidi, ili kuhakikisha mashauri yanayofikishwa Mahakamani yanamalizika kwa wakati.

Wito huo umetolewa leo na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Pangani Mjini Bwana Jordan Abraham kwenye Mazungumzo Maalum na kituo hiki, ambapo amesema kuwa ni muhimu kuwekeza nguvu nyingi katika kuhakikisha mashauri yanayofika kwenye ngazi ya Mahakama yanamalizika kwa wakati, kwani licha ya kupatikana kwa haki, kuna okoa muda na fursa ya kufanya shughuli za kujiingizia kipato.

 Sasa jambo linapokuwa limeisha kwa wakati tafsiri yake ni kwamba huyu mtu anapata fursa ya kuweza kupanga kufanya mambo yake mengine, kwa hiyo kuanzia mwananchi wa kawaida niwaombe tushirikiane na wadau hawa wenye kupewa mamlaka ya kufanya uchunguzi wa mashauri mbalimbali, lakini pia vyombo vyetu vya uchunguzi navyo vifanye kazi zao kwa weledi kwa kuzingatia sheria na taratibu na ukomo wa muda uliowekwa kisheria ili kuzipa urahisi mahakama zetu ziweze kufanya hayo maamuzi kwa wakati na hatimaye haki iweze kuonekana sio tu kutendekea bali pia ionekane imetendeka na imetendeka kwa wakatialisema  Hakimu  JordanAbraham

Bwana Jordan ameongeza kuwa tukiwa ndani ya wiki ya Sheria itakayofikia tamati tarehe 6 mwezi huu wa pili, pia maadhimisho hayo yataambatana na utoaji wa elimu kuhusu masuala mtambuka ya kisheria, kulingana na kauli mbiu ya mwaka husika, ambapo mwaka huu wa 2019 maadhimisho hayo yamebebwa na kauli mbiu isemayo “UTOAJI WA HAKI KWA WAKATI,,,WAJIBU WA MAHAKAMA NA WADAU”.

Hata hivyo amezungumzia namna walivyojipanga kuadhimisha wiki hiyo ya Sheria kwa kutembelea maeneo mbalimbali kutoa elimu, kuhusu namna njema ya wananchi kuzifikia mahakama kwa urahisi na kupata haki zao.

Tumejipanga vyema kama ilivyo ada yetu kwa kila mwaka, na kipaumbele chetu kikubwa ni kutoa elimu ya sheria. Jana tumekwenda kwenye shule mbalimbali za msingi na secondary ambako tumepata fursa ya kukutana na hadhara ya wanafunzi na kuweza kuwaelimisha kuhusiana na mambo kadha wa kadha ya kisheriaAlisema  Hakimu Jordan Abraham

Maadhimisho ya Wiki ya Sheria, mbali na kuadhimishwa kwa kutoa elimu mbalimbali kuhusu masuala ya kisheria yanayotatiza, pia inaashiria kuanza kwa Mwaka mpya wa Mahakama.

No comments

Powered by Blogger.