WANAKIKUNDI CHA UPENDO ENEO LA BOZA WALALAMIKIA HUDUMA YA MAJI KWENYE KILIMO CHA MBOGAMBOGA



Wajumbe wa kikundi cha UPENDO kinachojihusisha na shughuli ya kilimo cha mbogamboga  katika kijiji cha Boza wameelezea kuathiriwa na kitendo cha mamlaka ya maji mjini Pangani kutofungua maji kwa wakati pamoja na mifugo kuingizwa katika bustani zao hali inayosababishaa mbogamboga hizo kukauka.

Wakielezea kuhusu changamoto zinazowakabili wakati walipotembelewa na mwenyekiti wa kijiji hicho wajumbe hao wamesema kuwa upatikanaji wa maji umekuwa sio wa uhakika kwa sababu utaratibu wa kupata maji ni siku tatu kwa wiki lakini kuna baadhi ya wasimamizi hufungulia maji kwa muda mfupi na kupelekea athari za kupungua kwa kiwango cha uzalishaji wa mazao huku wakilazimika kulipia bili ya maji kila mwez.

Aidha mbali na changamoto ya utokaji wa maji kuwa siyo mzuri wanakikundi hao  wamesema uingizwaji wa mifugo katika bustani zao nayo imekuwa ni changamoto inayorudisha nyuma ukuaji wa mazao yao  na kupelekea kupata mavuno machache ambapo wamemuomba mwenyekiti wao awasaidie kutatua changamoto hizo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji hicho Bwana SHABANI SUFIANI MUSSA amewapongeza wanakikundi hao kwa kuanzisha mradi huo na kusema changamoto walizompa atazifanyia kazi kwa kufika kwa meneja wa mamlaka ya maji  mjini Pangani ili ikiwezekana afike naye katika mashamba hayo kwa ajili ya kutatua kero hiyo akisema wanakikundi hao wamekuwa wakilipa bili ya maji wakati huduma hawaipati kwa usahihi.

No comments

Powered by Blogger.