GARI KUACHA NJIA NA KUTUMBUKIA MTO PANGANI.



Gari moja aina ya MITSUBISH-CANTER yenye namba za usajili T 336 AAE mali ya Bwana MRISHO HEMEDI BAKARI, limeacha njia na kutumbukia katika Mto Pangani eneo la CASTAM palipo na Bandari ya Pangani.

Akithibitisha tukio hilo Mkuu wa Polisi Wilaya ya Pangani Bi Christina Musiani amesema kuwa tukio hilo limetokea leo Desemba Mosi 2017 majira ya saa Tano na Nusu Asubuhi, baada ya kondakta wa gari hilo Ally Hemedi mwenye umri wa miaka 23 alipokuwa akiligeuza gari hilo mara baada ya kumaliza kupakua Machungwa waliyokuja nayo kutoka Wilayani Muheza.


Aidha Mkuu huyo wa Polisi Pangani amesema kuwa pamoja na ajali hiyo kutosababisha madhara yoyote kwa Binaadamu, imesababisha uharibifu wa gari hiyo huku kijana Ally Hemedi ambaye ni Kondakta wa gari hilo akitokomea kusipojulikana hadi sasa.

Leo desemba mosi gari aina ya Mitsubish Canter T 336 AAE imeacha njia na kutumbukia katika mto pangani eneo hilo la Kastam ilipo Bandari ya Pangani baada ya kondakta wa gari hili alipokuwa akiligeuza mara baada ya kumaliza kupakua machungwa waliyokuja nayo kutokea Wilayani Muheza ili aweze kulipaki vizuri tayari kwaajili ya kuondoka”


“Pamoja na kusababisha uharibufu katika gari hilo tunashukuru Mwenyezi Mungu ajali hiyo haikusababisha madhara yoyote kwa binaadamu, tayari gari hiyo imeshatolewa na iko kituoni kukaguliwa na taratibu nyingine za kisheria zinaendelea, na kijana Ally Hemedi ambaye ni Kondakta wa gari hilo ametoroka hatujui amekimbilia wapi hadi sasa’ amesema Mkuu wa Polisi Pangani Bi Christina Musiani.
 


 
Katika hatua nyingine Bi Musiani ameongeza kuwa wakati wote Madereva wa vyombo vya moto wanapaswa kuwa makini, huku akitoa wito kwa madereva wote kupunguza Mihemko ya Mwisho wa Mwaka akisema baada ya Mwaka kumaliza, kuna Mwaka Mpya unaokuja hivyo maisha ni lazima yaendelee.

“Wakati wote lazima wazingatie usalama wa barabarani, tunapoendesha vyombo vya moto tusiangalie ufaghari au umaarufu Fulani kwamba unaweza kukimiliki chombo cha moto, lakini kikubwa ni kuangalia kwamba vile vyombo vimetengenezwa na binaadamu na wewe unahitaji kuishi” Amesema Bi Musiani na kuongeza kuwa

“Kwa hiyo madereva tuthamini sana nafasi tulizopewa kuishi na tuwe makini kwa kufuata sheria za barabarani, pia mihemko ile ya mwisho wa mwaka tuipunguze kwasababu baada ya mwaka kuisha tunauanza mwaka mwengine lazima maisha yaendelee tuzingatie na tuwe makini katika matumizi ya barabarani” Amesisitiza Bi Musiani.

Katika eneo hilo la KASTAM ilipo Bandari ya Pangani ni mara ya kwanza ajali kama hiyo kutokea, ambapo tukio hilo limezua taharuki kwa wapita njia pamoja na wapakiaji na wapakuaji mizigo eneo hilo.

No comments

Powered by Blogger.