SHIRIKA LA UZIKWASA LAKUTANA NA WADAU WA ELIMU PANGANI



Shirika La Uzikwasa lililopo wilayani  Pangani limekutana na kuzungumza na baadhi ya wadau wa elimu kwa kwa ajili ya kupata mrejesho wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazofanywa na shirika la Uzikwasa kwa kushirikiana na wadau hao.

Akizungumzia kuhusu mafanikio waliyofikia Mwenyekiti wa Kamati ya shule ya msingi Kwakibuyu Bwana SAMWELI DENIS amesema kuwa wamejitahidi kutatua changamoto mbalimbali kama vile ya uchache wa walimu kwa kushgirikisha wadau wa elimu waliopo katika eneo hilo.

’Nafikiri kuna mambo tumeyafanikisha kuna mambo bado kwa sababu yapo kama mambo manne au matano yaani kuna kuwepo kwa kujitahidi kuwepo chakula shuleni, nyumba za walimu, ujenzi vyoo na tumeongea na uongozi wa amboni plantation na yapo baadhi ya majengo wameyakarabati’’ amesema Samweli.

Aidha kutokana na mfumo salama wa kuripoti matukio ya ukatili kwa watoto bwana Samweli amesema wamelazimika kugawana majukumu na wajumbe wa kamati yake  kufuatilia matukio ya ukatili kwa watoto.
’Mfumo tumetengeneza kwa sisi wenyewe wana kamati kwamba kama utasikia jambo ufuatilie wewe mwenyewe kimnywa kimnywa na baada ya hapo tunaitisha kikao na kujadili ili tuangalie namna ya kulifanyia ufumbuzi kwa ujumla’’ amesema Samweli.

Kwa upande wake Mwezeshaji kutoka shirika la Uzikwasa Bwana Kennedy Mashema amesema zoezi limekwenda vizuri huku miongoni mwa makubaliano katika zoezi hilo ni kamati Kutembeleana, kufuatilia Kesi za ukatili kwa mfumo salama na kuchukua hatua stahiki.

‘’Katika kutathimini utendaji wa wadau imekuja ikaonekana kwamba kuna masuala inabidi yaangaliwe kwa kina kwa mfano ushirikiano kati ya kamati na walimu kwa maana ya matroni na patroni ili tuone namna ambavyo wanaweza kutatua matatizo ya kijinsia, sasa kuna matukio mengi sana ya ukatili kama shirika tukaona namna bora ya kuyapata ni kuweka huu mtandao wa uripotiji matukio’’ amesema Kennedy.

Zoezi la kukutana na wadau wa elimu wilayani Pangani  litaendelea leo kwa kanda ya kaskazini ya mto Pangani ambapo wawezeshaji hao watakutana na wadau katika kijiji cha Msaraza.

No comments

Powered by Blogger.