JESHI LA POLISI PANGANI LATOA TAHADHARI KUELEKEA SIKUKUU ZA KRISMASS NA MWAKA MPYA

Kamanda wa polisi wilayani Pangani Bi Christina Musiyani, amewataka wananchi wilayani humo kuzingatia suala la usalama wao pamoja na mali hasa katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za Krismass na Mwaka mpya..

Akizungumza na PANGANI FM mapema jioni ya leo, Kamanda Musiyani mbali na kuwataka wananchi kutii sheria, pia amesema kuwa jukumu la kulinda amani na usalama ni la wananchi wote hivyo ni vyema kila mtu akawa mlinzi wa mwenzake

"Jukumu hili sio la jeshi la polisi pekee, ndio maana tuna dhana ya ulinzi shirikishi, katika kuelekea sikukuu hizi za sikukuu ya Krismass na Mwaka Mpya ni vyema kila mmoja akawa mlinzi wa mwenzake kwani sikuku zinaweza kuwa chanzo cha uhalifu, lakini pamoja na yote jeshi la polisi tumejipanga kukabiliana na kila uhalifu utakaojitokeza" alisema Musiyani.

Kamanda Musiyani pia amewataka wageni wanaokuja kutembelea ufukwe wa Bahari ya Hindi eneo la Pangadeko hasa katika kipindi cha Sikukuu, kujiepusha na masuala ya uhalifu na pia kujisitiri miili yao kwa kuwa Pangani bado inaheshimu mila na utamaduni ulipo.

"Wageni tunawakaribisha, tunajua wanaipenda Pangani, lakini nawaomba wajisitiri, sisi Pangani tunamcha Mungu sana, pia hatuhitaji uhalifu wa aina yoyote, na mwisho hata wakienda kwenye kumbi za starehe basi ustaarabu uwepo" alisema kamanda Musiyani

Wito huo kutoka kwa Kamanda wa jeshi la polisi wilayani Pangani Bi Christina Musiyani unakuja ikiwa zimesalia siku nne kabla ya waumini wa dini ya Kikristo duniani kote kuungana na kusherehekea sikukuu ya Krismass ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo tarehe 25.

No comments

Powered by Blogger.