"MFUME DUME UNAZOROTESHA MIPANGO YA MAENDELEO KWA WANAWAKE" BI HALIMA



Kuendelea kukumbatiwa kwa Mfumo Dume Wilayani Pangani kumeelezwa kusababisha mikwamo na changamoto za kiungozi kwa wanawake, pasi na kuangalia ujasiri na uwezo wao katika kufanikisha mipango ya kimaendeleo.

Akizungumza na kituo hiki Bi Halima Hamisi ambaye ni mshindi aliyeshika nafasi ya tatu katika shindano la kutafuta mama bora wa mfano wa kuigwa Wilayani Pangani 2017, amesema kuwa mwanamke anapojiamini anaweza kufanya mengi yenye faida kwenye jamii yake, lakini baadhi ya watu kuendelea kuukumbatia mfumo dume kunasababisha kufinika uwezo walionao.

Aidha Bi Halima amesema kuwa katika uwezo wake mumewe anahusika kwa kiasi kikubwa kwani ni tofauti na wanaume waliowengi, akimsifu kwa kumtia moyo na uvumilivu alionao. 

“Kwa kweli suala la Uongozi Wilayani Pangani, tena sijui niseme mkoa wote wa Tanga! Yani changamoto ni nyingi lakini nashukuru nipo na mume anayejitambua, laiti ningekuwa na mume asiyejitambua sijui ingekuwaje. Ila nashukuru mume wangu anajitambua ni mume anayejielewa, ukweli kwa hilo napenda kumshukuru sana. Ananiunga mkono ni mwanaume mvumilivu sana” amesema Bi Halima. 



“Mwanamke ukijiamini unaweza na usipo jiamini kila siku utabaki kuwa nyum. Mimi nimejiamini na kweli nimeweza kwani hata nilipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya shule nilifanikisha upatikanaji wa maji shuleni tatizo ambalo kwa muda mrefu liliwatesa wanafunzi, pili nilisimama kidete na kulishughulikia tatizo la vyoo shuleni hapo na hadi sasa ukiachilia vyoo, kuna madarasa mawili ya kisasa pale shule ya msingi mivuni ukifika utayaona mazuri”amesisitiza Bi Halima Mama Bora Wilayani Pangani 2017.
 
Pamoja na hilo amegusia changamoto nyingine inayomkabili kama mkwanamke ni itikadi za kisiasa akisema amewahi kuondolewa kwenye nafasi ya uongozi katika kamati ya maji kutokana na kutofautiana na wengine kiitikadi, lakini bado amehakikisha kukazana akisema yapo mengi kwenye jamii yanayopaswa kushughulikiwa.

“Kweli hilo ndio linalotuathiri mivunoni, unapokuwa wewe ni mwanachama wa chama kingine, utatafutiwa mbinu za kila aina, watu wanaunda visababu, hata katika uongozi utatolewa tu hilo ni lazima yani hapa nasema wala sifichi, mimi kule kwenye kamati ya maji nimetolewa bila sababu ya msingi lakini bado nakazana na mengine kwani kwenye jamii yapo mengi yanayopaswa kushughulikiwa. Amesema Bi Halima.



Amemalizia kwa kuwashauri wanawake wengine kujitambua na kutobaki nyuma, wala kuogopa watu wanasemaje badala yake wahakikishe wanaondoa tofauti zao nakushikamana kuijenga jamii kwa pamoja. 

“Ushari wangu kwa wanawake wenzangu kwa kweli tujitambue, na utakapotambua kuwa wewe ni mwanamke na unaweza usibaki nyuma na wala usiogope kwamba yule atasemaje! kwani mti unaopigwa mawe ni mzuri, kwa hiyo wote inatakiwa tuheshimiane, tukubaliane, tufanyekazi kwa pamoja, kwani tukishaanza kuleta ukwanini hatutajenga mana sisi wote ni jamii moja, tuondoe zile tofauti za ukwanini” amesema Bi Halima.

Bi Halima Hamisi ni mwenyeji katika kijiji cha Mivumoni Wilayani Pangani, ambaye ameshika nafasi ya tatu kama mama bora wa mfano wa kuigwa 2017 katika shindano la kutafuta kamati bora ya kudhibiti ukimwi jinsia na uongozi VMAC-Kijana Bora na Mama Bora wa Mfano wa kuigwa kwa mwaka 2017, tamasha lililofanyika katika kijiji cha Msaraza Wilayani humo Desember 16 mwaka huu.

No comments

Powered by Blogger.