VITUO VIWILI VYA MAFUTA PANGANI VYAFUNGIWA NA TRA



Mamlaka ya mapato mkoani Tanga TRA leo imevifungia vituo viwili vya kujazia  mafuta vilivyopo wilayani Pangani, kutokana na vituo hivyo kutotumia mashine za kutolea risiti za EFDs.

Akizungumza na Pangani fm Afisa kodi Msaidizi  na Msimamizi wa mashine za EFDs kutoka mamlaka ya mapato Tanzania Mkoa wa TANGA Bwana Buruba Kanuda, ameeliza sababu za kuvifungia vituo hivyo vya mafuta kutokana na kushindwa kutekeleza agizo la kufunga mashine za EFDs, na kwamba watazifungulia hadi pale vituo hivyo vitakapokamilisha utaratibu wa kufunga mashine hizo.

‘’nakumbuka kwamba hawa wenye vituo vya mafuta walipewa maelezo ya kufunga mashine maalumu ambazo zinatumika kwa watoa mafuta kama hivi lakini wengi wao hawakufunga kwa wakati sasa vituo hivi vinafungwa na vitaanza kufanya kazi hadi pale watakapofunga mashine’’ amesema Bwana Buruba.


Wakizungumzia hali hiyo madereva wa Bodaboda Wilayani humo, wametanabaisha kuwa kufungiwa kwa vituo hivyo itaifanya baishara yao kuwa ngumu kutokana na wao kutegemea zaidi bidhaa hiyo.

‘’hii hali nilipofika hapa nilikuwa sielewi na nimekuja hapa ili kujaza mafuta lakini cha kushangaza vituo vyote vimefungiwa hali hii itatugharimu sana sisi madereva wa boda boda kwa sababu sisi tunategemea mafuta ili tufanye kazi lakini kwa hili ndo tumeshakwama tena’’ amesema mmoja wa boda boda.

Mashine EFDs  ni mashine zilizotengenezwa kwa ajili ya kutumika katika biashara kwa lengo la kudhibiti usimamizi kwa ufanisi katika maeneo ya uchambuzi wa mauzo, na mfumo wa udhibiti wa mali na ambao unafuata masharti yaliyoelezwa na sheria.


No comments

Powered by Blogger.