NGUVU YA PAMOJA NDIO CHACHU YA KUTOKOMEZA UKATILI WA KIJINSIA KIJIJI CHA KIMANG'A WILAYANI PANGANI
Nguvu ya Pamoja katika kutekeleza mipango ya
kimaendeleo kijiji cha Kimang’a, inaelezwa kuwa ndio mwarobaini utakaokomesha
vitendo vya ukatili wa kijinsia kijijini hapo.
Wakizungumza mapema hii leo katika kipindi cha
ASUBUHI YA LEO kinachorushwa na kituo hiki, baadhi ya wajumbe wa kamati ya
kudhibiti Ukimwi Jinsia na Uongozi ya kijiji cha Kimang’a wamesema kuwa siku za
nyuma hawakuweza kufanikiwa kutokana na kukosekana Ushirikiano na Umoja
miongoni mwao.
Aidha Bwana Daudi Bushishi ambaye ni Katibu Msaidizi
kwenye Kamati hiyo, amesema kuwa siri ya kamati yao kupata mafanikio ni umoja,
maelewano baina yao pamoja na kushikamana tangu wapopatiwa elimu ya uongozi wa
mguso.
Naye Bi Maria Peter ambaye ni mmoja ya wajumbe
katika kamati hiyo, kufuatia mkasa aliowahi kupitia wa kukatishwa masomo
kutokana na vishawishi alivyokutananavyo, ametumia nafasi hiyo kuwaonya mabinti
wengine ambao kwasasa wanakumbana na vishawishi hivyo kutokubali kudanganyika.
“Kwa kweli roho yangu inauma sana. Wasichana
wenzangu, wanawake wenzangu na hata wanafunzi kuweni makini, mimi kama Maria
maisha yangu ya pale kijijini kwetu Kimang’a watu wanayaelewa, nilivunjiwa
masomo baada ya kushawishiwa na vijana na baadae kupewa ujauzito, ndoto za
kielimu zikaishia hapo. Sasa nawaambia bila elimu sasa hivi sawa na bure,
unachotakiwa ni kusoma hayo mambo mengine utayakuta, hao wanakulaghai tu!
Wakikukuta watapuka elfu moja, elfu mbili mwisho wa siku watakuvunjia ndoto
zako, nawausia kuweni makini” Amesisitiza Bi Maria.
Bi Maria amemalizia kwa kusema ili kukomesha kabisa
vijana waliojikoki kukatisha ndoto za kielimu kwa watoto wakike, ushirikiano
wao ndio utakuwa mwarobaini tosha kwa kuwakamata, na kuhakikisha wanaozea
katika mikono ya sheria.
“Tutakapo wakamata tuwafikishe katika vyombo vya
sheria, na baada ya kuwafikisha huko isiishie hapo, bali tuhakikishe wote
walioshikwa baada ya kubainika kazi yao ilikuwa ni kuwaharibia maisha watoto wa
kike, wanaozea katika mikono ya sheria, nadhani huu utakuwa mwarobaini hasa wa
kukomesha tabia mbovu za watu hao katika kijiji chetu”Amesema Bi Maria Peter.
Kamati ya Kudhibiti Ukimwi Jinsia na Uongozi VMAC ya
kijiji cha Kimang’a, imeshika nafasi ya 7 katika tamasha la kutafuta kamati
bora mwaka 2017, kutoka nafasi ya 22 iliyokamata mwaka 2016, nah ii ni kutokana
na kukua kiutekelezaji wa mipango mkakati.
No comments