JESHI LA POLISI PANGANI LASISITIZA AMANI NA USALAMA KAMPENI ZA UDIWANI KATA YA MADANGA
Jeshi la polisi wilayani Pangani limesema kuwa
halitamvumilia mtu yeyote mwenye nia ya kuvuruga kampeni za uchaguzi mdogo wa
udiwani, unaondelea katika kata ya Madanga wilayani humo.
Akizungumza na Pangani Fm, kamanda wa polisi
wilayani Pangani Bi Christina Musyani amesema kuwa, mbali na kubaini makundi
yanayotaka kuwatisha wanawake wasiende kupiga kura, pia amesisitiza suala la
amani na usalama wakati wote wa kampeni, huku jeshi la polisi likijipanga kushiriki
katika kila mkutano.
“Yako makundi yanataka kuwatisha wanawake wasije
kujitokeza kwenda kupiga kura! Hapana, uchaguzi ni uhuru na ni demokrasia ya
kila mmoja, kila mmoja anatakiwa kutumia nafasi hii kwaajili ya kumchagua yule
anayemtaka na anadhani kwamba atasaidia katika kuleta maendeleo yake na atafurahia
uongozi wa kiongozi huyo”. Amesema hivyo Kamanda Musyani na kuongeza kuwa…..
“Kila ambapo kuna ratiba kutakuwa na mikutano
tutakuwepo, kuhakikisha kampeni zinakwenda salama” Amesema Kamanda Christina
Musyani
Kamanda Musyani pia amewataka wagombea wanaowania
nafasi ya udiwani katika kata hiyo, kunadi sera zao kwa kufuata utaratibu
pamoja na miongozo ya kampeni iliyowekwa ili kujiepusha na uvunjifu wa amani
pamoja na kulinda misingi ya demokrasia iliyopo hapa nchini.
“Kila anaeuza sera, auze huku akiangalia miongozo ya
kampeni ikoje mpaka uchaguzi, aangalie pia je sheria zikoje, kwa hiyo tutumie
nafasi yetu, ni uhuru wetu, demokrasia yetu lakini isilete madhara, kila mwenye
kampeni afanye kwa usalama na amani na hatimaye tujetufike uchaguzi na hata
baada ya uchaguzi tuendelee kudumisha amani yetu na ushirikiano wa kuijenga Pangani
yetu. Amese kwa msisitiza Kamanda Musyan.
Kwa upande mwengine Kamanda Musyani hakusita
kuwashauri wananchi wa Madanga kujiepusha na kampeni za ushawishi na mihemko
kutoka nje ya eneo lao, kwa kuwa wao ndio wanaojua hali halisi na diwani
wanayemtaka ambaye atakuja kushirikiana na madiwani wengine kwa lengo la
kuiletea Pangani maendeleo.
“Huu ni uchaguzi mdogo wa ndani ya kata kwaajili ya
kumtafuta diwani wa Madanga, kwa maana hiyo hatutarajii kwamba ushawishi mkubwa
utoke nje, ni wanaMadanga ndio ambao wanafahamu hali halisi iko vipi, ukiacha
wanaMadanga pia kuna wanaPangani kwahiyo hatutarajii kwamba ushawishi utoke
nje, vurugu zije kutoka nje, sisi tunafahamiana wanaPangani na tunajua kwamba tukipata kiongozi bora Madanga
basi Pangani itasonga mbele kwa sababu atashirikiana na madiwani wenzake, lugha
itakuwa moja, Pangani itaenda mbele”. Amesema Kamanda wa Polisi (W) Pangani
Christina Musyan.
No comments