HATIMAE KITUO KIMOJA CHA MAFUTA PANGANI CHAANZA KUFANYA KAZI
Siku tano baada ya
Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA mkoa wa tanga kuvifungia vituo viwili vya Mafuta
mjini Pangani kwa kosa la kutotumia mashine za kutolea risiti za EFDs hatimaye
leo kituo kimoja cha Mafuta cha TOC mjini humo kimeanza kutoa huduma baada ya kufunga
mashine hizo.
Akizungumza na Pangani
fm Mkurugenzi wa kituo hicho Bwana Swaleh Amar Abdallah amesema baada ya kufungiwa kutotoa huduma waliwaita mafundi
wanaohusika na ufungaji wa mashine hizo za EFDs na Mapema leo Januari 10, 2018
wameanza kutoa huduma kama kawaida.
“Huduma tumeianza siku
ya leo saa tatu asubuhi na ilisitishwa na TRA kwa sababu ya kutofunga mashine
za EFDs lakini tumejitahidi kadri ya uwezo wetu kurekebisha hilo tatizo
tumewaita mafundi kutoka Tanga na Dar es Salam kwa hiyo walikuja hapa Pangani
kukaa kwa muda kama siku mbili hivi, tunashukuru Mungu hapa kila kitu kipo
vizuri na huduma ipo masaa 24” Amesema Bwasema na Swaleh ambaye mkurugenzi wa
kituo hicho.
Mbali na kuelezea
walivyoathirika baada ya kufungiwa kutotoa huduma hiyo Bwana Swaleh amesema
tangu asubuhi walipoanza kuzitumia mashine hizo za EFD hakujajitokeza changamoto yoyote ya kiufundi
kupitia mashine hizo.
“Kutuathiri kweli
imetuathiri kwa sababu tuna wateja wetu wengine kutoka Kipumbwi huko kwa hiyo
unakuta yani akija mpaka hapa halafu akakosa huduma ya mafuta yani hajisikii
vizuri anatuona kama ni uzembe wa kazi, kusema kweli maendeleo ni mazuri na
bado hatujaona changamoto yoyote kwa sababu hizi kadi tulizoweka ni mpya na hii
mashine tuliyofunga ni mpya umeona kwa hiyo hatujapata changamoto yoyote” Amesema
Bwana Swaleh Abdallah.
Kwa upande wao wateja
wa mafuta katika kituo hicho wameelezea kufurahishwa na kurejea kwa huduma ya
mafuta wakisema kituo hicho kilipofungiwa walipata adha kubwa ya kufuata huduma
hiyo wilaya jirani ya Muheza na kusababisha waendashaji wa vyombo vya moto
hususan pikipiki kulazimika kununua bidhaa hiyo kwa bei ya juu.
“Tumefurahi sana kupata
huduma hii ya mafuta, walipofungiwa tulipata shida sana kwa sababu tulikuwa
tuna nunua mafuta kwa shilingi elfu tatu ambayo ilikuwa inatugharimu sana”. Amesema
mmoja wa waendesha pikipiki mjini Pangani.
Kituo cha TOC ni
miongoni mwa vituo viwili vya mafuta hapa mjini Pangani vilivyofungiwa na
mamlaka ya Mapato Tanzania mnamo tarehe 5 Januari mwaka huu kwa kosa la
kutotumia mashine za kielektroniki za EFDs.
No comments